• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Ole Kina na Buzeki kujiunga na ANC, adokeza Malala

Ole Kina na Buzeki kujiunga na ANC, adokeza Malala

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala Jumapili alifichua kuwa Seneta wa Narok Ladema Ole Kina na aliyekuwa mgombea wa ugavana katika Kaunti ya Uasin Gishu Zedekiah Bundotich Buzeki wamekubali kufanya kazi na chama cha Amani National Congress (ANC).

Akiongea baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Church of God mtaani South B, alisema wanasiasa hao wawili ni miongoni mwa vingozi wengi ambao wameamua kuunga mkono azma ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ya kuingia Ikulu, 2022.

“Hivi karibuni mtaona tukitembea na Mheshimiwa Zedekiah Bundotich maarufu kama Buzeki. Nimemfikia na amekubali kuungana na timu yetu. Vile vile, nimemfikia Seneta wa Narok Ladema Ole Kina kwani ni mmoja wa wale ambao wako njiani kujiunga nasi na tuko tayari kumkaribisha. Wote watatusaidia kuendeleza ajenda ya Musalia Mudavadi kwa Wakenya,” Bw Malala akasema.

Seneta huyu wa Kakamega alikuwa mstari wa mbele katika kampeni kuelekea uchaguzi mdogo wa Matungu na amekuwa akipaza sauti kuhusu ndoto za Mudavadi za kuingia Ikulu baada ya kuridhiana kisiasa na kiongozi huyo wa ANC mwaka 2020.

Bw Malala na Bw Mudavadi hawajakuwa wakielewana kisiasa tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya seneta huyo kuonekana kuegemea zaidi upande wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

Lakini mwaka 2020 wawili hao waliridhiana na sasa Malala amejitokeza kuwa mpigaji debe mkubwa wa ndoto ya Mudavadi ya kuwa Rais wa tano wa Kenya, Rais Kenyatta akitarajiwa kustaafu mwaka 2022.

You can share this post!

Cyrus Ruru afariki na kuacha maswali kuhusu kifo cha diwani...

Messi afunga mawili akiweka rekodi ya kuchezea Barcelona...