Uhuru asifu Pombe kwa kuhepa ukopaji

CHARLES WASONGA NA PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumatatu alimsifu aliyekuwa rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli kama mtu aliyeonyesha kuwa nchi za Afrika zinaweza kufadhili maendeleo bila kukopa pesa kutoka mataifa ya kigeni.

“Kwa miaka michache, Rais Magufuli ameonyesha kuwa Mwafrika anaweza kufadhili na kusimamia miradi ya maendeleo bila kutegemea mataifa ya wazungu. Hii ni kwa sababu alikuwa kiongozi aliyeweka mbele masilahi ya watu wake,” akasema Rais Kenyatta akihutubu wakati wa ibada ya wafu ya mwendazake Magufuli katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

“Alituonyesha kuwa sisi kama Waafrika tuko na uwezo wa kujikomboa kutokana na kutegemea wageni. Alionyesha kuwa tuko na uwezo kama Waafrika wa kusimamia chumi zetu na kuhakikisha kuwa watu wetu wamepata haki,” akasema Rais Kenyatta.

Rais Magufuli alifanya miradi mingi ya maendeleo bila kutegemea ufadhili wa kigeni, kinyume na Rais Kenyatta ambaye chini ya uongozi wake madeni ya Kenya yameongezeka kwa kiwango kikubwa.

Mradi unaotambuliwa zaidi ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayotumia umeme kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma ya umbali wa kilomita 700, ambayo inafadhiliwa na raslimali za Watanzania bila mkopo kutoka nje.

Mradi wa SGR ya Kenya wa umbali wa kilomita 480 kutoka Mombasa hadi Nairobi ulijengwa kwa mkopo wa Sh327 bilioni kutoka China.

Chini ya utawala wa Rais Kenyatta, deni la Kenya limeongezeka kutoka Sh1.8 trilioni alipochukua madaraka kutoka kwa Mzee Mwai Kibaki hadi Sh7.2 trilioni kufikia mwishoni mwa mwaka 2020.

Utawala wa Mzee Kibaki ulikuwa umechukua mwelekeo kama wa Magufuli wa kufadhili miradi mingi ya maendeleo kutokana na ushuru wa ndani mwa nchi badala ya kukopa, mchakato ambao ulibadilika chini ya utawala wa Jubilee.

Miradi mingine aliyokuwa akiendesha marehemu Magufuli ni upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na mradi wa kilimo wa Mkunazi Agriculture City mjini Zanzibar, unaofadhiliwa kwa pesa za malipo ya uzeeni.

Mingine ni Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam na bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga.

Wakati wa ibada ya mazishi hapo Jumatatu, marais waliohutubu walimmininia sifa Rais Magufuli wakimtaja kama kiongozi mchapa kazi na aliyejitolea kupambana na ufisadi kwa manufaa ya watu wake.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Felix Tshisekedi (Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), marais hao walimsifia mwendazake kama kiongozi aliyependa nchi yake na ambaye hakutegemea misaada ya kigeni kufanikisha maendeleo.

“Sisi kama viongozi wa Afrika tumejifunza mengi kutokana na uongozi wa ndugu yetu Magufuli, ambaye alifaulu kwa kiwango kikubwa kupambana na ufisadi, ambao ni kansa ya maendeleo barani Afrika,” akasema Tshisekedi.

Rais huyo wa DRC pia alisifu rekodi ya maendeleo ya marehemu Magufuli katika kipindi cha miaka sita ambayo aliongoza Tanzania.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na marais Kenyatta, Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini) na Filipe Yasinto Nyusi (Musumbiji).

Wengine waliohutubu ni Azali Assoumani (Visiwa vya Comoros), Lazarus Chakwera (Malawi), Edgar Lungu (Zambia) na Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe).

Rais Ramaphosa alisema marehemu Magufuli hakupenda kusafiri mataifa ya ng’ambo kwa sababu alitaka kusalia nyumbani kuwahudumia watu wake.

“Rafiki yangu hakupenda kusafiri nje ya nchi. Wakati mmoja nilidhani aliogopa kusafiri kwa ndege, lakini nilipozungumza naye alinihakikishia kuwa alitaka kukaa nchini Tanzania kuwahudumia watu wake badala ya kusafiri kila mara,” akaeleza.

“Hii inaonyesha kuwa marehemu Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyependa taifa lake na bara la Afrika kwa ujumla,” Rais Ramaphosa akaongeza.

Rais huyo wa Afrika Kusini pia alimtaja mwendazake kama kiongozi ambaye alihusudu na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Habari zinazohusiana na hii