• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Familia yaangamia ikimlilia Magufuli

Familia yaangamia ikimlilia Magufuli

Na ALFRED ZACHARIA

WATU watano walifariki katika rabsha iliyotokea jijini Dar es Salama mnamo Jumapili, wananchi wa Tanzania walipojitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa rais, John Magufuli.

Watano hao walikuwa watu wa familia moja ambayo sasa imebaki ikiomboleza.

Maafisa wa usalama na wahudumu wa mashirika ya kutoa huduma za dharura walikuwa na wakati mgumu kudhibiti maelfu ya watu waliojaa katika uwanja wa michezo wa Uhuru wakitaka kutoa heshima kwa rais wao.

Watu kadha walizirai, huku ripoti zikionyesha kuwa wengine wengi walijeruhiwa katika purukushani zilizozuka katika uwanja huo.

Ni katika hali hiyo ambapo familia ya Mzee Mtuwa, mkazi wa kitongoji cha Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam, ilipoteza wapendwa wao.

Watano hao ni; Chris, mwenye umri wa miaka 11, Michael (8), Nathan (6), Natalia (5) na Suzan Ndana Mtua mwenye umri wa miaka 30.

Garald Mtuwa, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mzee Mtuwa alisema Suzan alikuwa shemeji yake na amemwacha mtoto mmoja na mumewe, Denis Mtuwa.

Alisema yaya ambaye alikuwa ameandamana na watano hao hajulikani aliko tangu Jumapili, mkasa huo ulipotokea.

“Hatujamwona tangu jana (Jumapili) hata baada ya kumsaka katika hospitali ya Temeke. Kwa hivyo, hatujui ikiwa alifariki au alitorokea kusikojulikana,” akasema.

“Waliwasili katika Uwanja wa Michezo wa Uhuru majira ya asubuhi. Walituma picha ambazo walipiga wakiwa uwanjani humo. Mwendo wa saa sita adhuhuri, shemeji yangu (mumewe Suzan) alimpigia Suzan simu lakini hakushika siku. Baadaye mtu aliichukua na kutujuza kuwa alikuwa amezirai,” akasema.

Duru zilisema huenda idadi ya waliokufa kwenye mkasa huo ikawa ya juu zaidi.

Kamanda wa Polisi jijini Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliahidi wanahabari kuwa atatoa taarifa zaidi kuhusu mkasa huo hivi leo.

Kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu wakati wa ibada ya wafu jijini Dar es Salaam mnamo Jumapili, hali ambayo inatajwa kuwa kiini cha mkanyagano uliopelekea baadhi ya watu kufariki na wengine kupata majeraha.

You can share this post!

KCPE yaanza kwa visa vya kujifungua

Serikali yaondoa kafyu katika eneo la Kapedo