• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Serikali yaondoa kafyu katika eneo la Kapedo

Serikali yaondoa kafyu katika eneo la Kapedo

Na MARY WAMBUI

SERIKALI Jumatatu iliondoa kafyu iliyokuwa imewekwa Kapedo kwa siku 30 kutokana na ukosefu wa usalama.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alisema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kurejesha utulivu katika eneo hilo la mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana.

“Nashukuru huduma ya serikali ya kitaifa na maafisa wa utawala ambao wamechangia katika kuleta amani Kapedo. Nashukuru pia msaada kutoka kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, Baringo na Samburu katika kudumisha amani,” alisema Dkt Matiangi.

Waziri alieleza kwamba sehemu ya ufanisi huo ni kukomesha waliokuwa wanaochochea vurugu.

Alisema wakati wa hali hiyo ya watu kutotoka nje ya nyumba kati ya saa kumi na mbili za jioni na kumi na mbili alfajiri, serikali ilifanikiwa kukusanya bunduki 53 zilizokuwa mikononi mwa watu bila leseni.

“Pia wachochezi na wazuaji vurugu kadhaa walikamatwa,” akasema waziri.

Dkt Matiang’i alisema kutokana na juhudi hizo, masomo yaliendelea na sasa mtihani wa kitaifa ulioanza jana unaendelea.

Kafyu iliyowekwa Januari 25 mwaka huu, ilikuwa njia ya kuwapa nafasi maafisa wa usalama wakusanye silaha kama vile bunduki zilizokuwa mikononi mwa wananchi.

Serikali iliweza kukomesha mikusanyiko yoyote ya watu katika eneo la Turkana Mashariki kata ndogo ya Tiaty Mashariki na Magharibi.

“Japo kafyu yenu imeondolewa, msisahau kuwa kafyu ya kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi asubuhi iliyowekwa na serikali bado inaendelea kuzingatiwa,” Dkt Matiangi alisema.

You can share this post!

Familia yaangamia ikimlilia Magufuli

Rais apigiwa makofi kwa kukatiza hotuba juu ya maombi