• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
VISABABISHI: Tatizo la damu kuganda mwilini si jambo geni katika masuala ya kiafya

VISABABISHI: Tatizo la damu kuganda mwilini si jambo geni katika masuala ya kiafya

Na LEONARD ONYANGO

WATAALAMU wanaonya kuwa tatizo la kuganda kwa damu linaweza kutokea mtu anapotumia dawa kupita kiwango kilichowekwa.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa hivi karibuni zinaonyesha kuwa dawa za kawaida za kupunguza maumivu, kama vile aspirin na ibuprofen, zinapotumiwa kiholela kupita kiasi, zinaongeza uwezekano wa damu kuganda mwilini hivyo kumweka mtumiaji katika hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo ghafla.

Kwa kuwa dawa za kupunguza maumivu hupatikana kila mahali, watu hununua na kuzitumia kiholela bila kupata ushauri wa daktari au kufuata maelekezo ya mtaalamu au yaliyo kwenye pakiti za hizo dawa.

Mamlaka ya Kuhakiki Usalama wa Vyakula na Dawa nchini Amerika (FDA) mnamo 2019, ilionya kuwa dawa ya tofacitinib inayotumiwa kutibu maradhi ya jongo (arthritis) inaweza kusababisha damu kuganda mwilini iwapo mgonjwa atatumia miligramu (mg) 10 mara mbili kwa siku. Badala yake FDA ilishauri kuwa dawa ya hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer itumike mg 5 mara mbili kwa siku.

Mbali na kutumia dawa, uzee, kuketi kwa muda mrefu, kulala kitandani kwa siku nyingi, unene kupindukia, kuvuta sigara na kansa vinaongeza uwezekano wa damu kuganda kwenye mishipa na kusababisha mshtuko wa moyo na hata kifo.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), japo tatizo hili linaweza kutokea kwa mtu wa umri wowote, wazee wa miaka 60 na zaidi wako kwenye hatari zaidi.

Kuketi kwa muda mrefu, haswa unaposafiri umbali mrefu, kunasababisha damu kutozunguka miguuni hivyo inaweza kuwa hatari kwa afya.

Tafiti pia zinaonyesha kuwa baadhi ya wanawake wanakuwa katika hatari ya damu kuganda wakati wa ujauzito. Hii ni kwa sababu mimba huongeza presha katika sehemu ya chini ya tumbo na miguu.

Lakini wataalamu wanasema kuwa tatizo hilo hutokea zaidi miongoni mwa akina mama ambao wamerithi kutoka kwa wazazi wao. Wanawake wanaweza kuwa katika hatari ya kupatwa na tatizo hilo hata miezi sita baada ya kujifungua.

Uvutaji sigara unaweza kusababisha damu kuzunguka kwa shida mwilini hivyo hali hiyo inaweza kusababisha damu kuganda.

Aina fulani za kansa huongeza viini ndani ya damu ambavyo pia vinaweza kusababisha damu kuganda, kulingana na wataalamu.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Corona: Chanjo ya AstraZeneca ni salama?

Lukaku kuongoza mashambulizi ya Ubelgiji dhidi ya Wales