• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
TAHARIRI: Wazazi wawachunge watoto na mitandao

TAHARIRI: Wazazi wawachunge watoto na mitandao

KITENGO CHA UHARIRI

ONYO la Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC) kwa wazazi kuwa wanafaa kutahadhari kuhusu mienendo ya watoto wao kwenye mitandao linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Kituo hicho kilitoa tahadhari hiyo Jumapili, baada ya kubainika kuwa makundi ya kigaidi yanatumia mitandao kuwasajili watoto ili kuwaingiza kwenye ugaidi.

Bila shaka, wazazi wanafaa kuzingatia tahadhari hiyo kwa umakinifu mkubwa, ikizingatiwa wanafunzi wengi wako kwenye likizo.

Mara nyingi, wanafunzi hutumia likizo kujifunza mambo mapya, hasa yale wanayozuiwa wakiwa shuleni.

Ni wakati huu ambao huutalii ulimwengu kwa kila namna. Miongoni mwa vifaa ambavyo huwa wanatumia kutimiza hayo ni simu, tarakilishi na vipakatalishi.

Kwa kuwa wazazi wengi huwa na shughuli nyingi za kikazi, ni wachache ambao hufuatilia vitendo vya wanao kwenye mitandao.

Pengo hilo huwapa baadhi ya wanafunzi wakati kufanya kila walitakalo. Kuna wale ambao hutumia mitandao hiyo kwa njia nzuri, kama vile kujiendeleza kimasomo ama kufuatilia yale yanayoendelea duniani.

Wengine hubadilishana mawazo na wenzao na kuvumbua mambo muhimu, ambayo baadaye huchangia sana ustawi wa nchi, hasa kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

Hata hivyo, kuna wanafunzi ambao hutumia mitandao hiyo kuwasiliana na watu wasiowajua, ama kuendeleza maovu kama vile masuala ya ugaidi na ngono. Ni kundi hilo ambalo limekuwa likilengwa na makundi ya kigaidi ama watu wenye nia mbaya kwao.

Baadhi ya vishawishi ambavyo hutolewa kwao ni ahadi ya kupewa fedha nyingi ili kuishi maisha ya kifahari na ya kuvutia.

Wengine huelezwa namna familia zao zitakavyosaidiwa kifedha ikiwa watajiunga na makundi hayo au kukubali itikadi zake.

Chunguzi kadhaa ambazo zimefanywa kuhusu kiini cha baadhi ya mashambulio ya kigaidi nchini, zimebaini yalipangwa na kutekelezwa na vijana walioingizwa kwenye makundi hayo kwa njia ya mtandao.

Cha kushangaza ni kuwa, baadhi yao walikuwa bado wanafunzi!

Bila shaka, huu ni wakati muhimu kwa wazazi kuwa waangalifu kuhakikisha wanao hawapotoshwi na kujiunga na makundi hayo.

Hili litahakikisha wanawapa mwongozo ufaao kuhusu namna ya kujiepusha na vishawishi hivyo.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Awadh hajasoma ila anasifika kwa kuongoza...

WARUI: Ni jukumu letu sote kuzuia wizi wa mitihani ya...