• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
WARUI: Ni jukumu letu sote kuzuia wizi wa mitihani ya kitaifa

WARUI: Ni jukumu letu sote kuzuia wizi wa mitihani ya kitaifa

Na WANTO WARUI

HUKU mtihani wa Darasa la Nane, KCPE ukiingia siku ya pili leo nao ule wa Kidato cha Nne, KCSE baadaye, serikali pamoja na wananchi wote tuna jukumu la kuhakikisha kuwa mitihani hiyo haichafuliwi kwa wizi.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na wizi wa mitihani kila mwaka, tabia iliyoongezeka zaidi wakati wa uongozi wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Prof Jacob Kaimenyi.

Katika wakati huo, wizi wa mitihani ulikuwa kama jambo la kawaida ambapo kiwango cha kuibia mitihani kilifika juu sana na kulazimisha serikali kulipiga darubini suala hilo la mitihani.

Ni hapo ambapo Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliteuliwa kusimamia wizara hiyo.

Kwa muda mfupi tu baadaye, tuliweza kuona mabadiliko makubwa sana; wizi wa mitihani ulipungua kwa kiasi kikubwa nayo matokeo ya mitihani yakapata thamani yake.

Tunakumbuka kuwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, KCSE ya mwaka wa 2016 yalipokelewa kwa mshtuko mkubwa baada ya wanafunzi 141 pekee kote nchini kupata alama ya A.

Hapo awali, matokeo kama hayo yangetoka katika shule moja tu!

Ni hapo ambapo wananchi walianza kurejeshe imani yao ambayo ilikuwa imetoweka katika elimu.

Baada ya hapo, wizi wa mitihani ukapungua kabisa kufuatia uangalizi mkali na hata sheria kali zilizowekwa.

Hata hivyo, baada ya waziri Matiang’I kuhamishiwa wizara ya Usalama wa Ndani, tetesi zilianza kusikika kuwa wizi huo wa mitihani unarejea tena polepole. Mwaka wa 2019, kulikuwa na kesi kadhaa za wizi wa mitihani.

Tuliweza kusikia kuwa kuna shule ambazo zilishirikisha walimu au wazazi katika wizi huo.

Unapofika wakati ambapo mwalimu au mzazi anamsaidia mwanafunzi kuibia mtihani, ina maana kuwa sheria zimelegezwa na wale waliochaguliwa kulinda mitihani hiyo wamelala.

Ninamshukuru sana afisa mmoja wa usalama ambaye alifichua njama ya kuibia mtihani katika mojawapo ya shulehumu nchini.

Ni tabia kama hizi za uajibikaji ambazo jamii yetu inastahili kukumbatia ili kuangamiza kabisa wizi huu wa mitihani.

Na sasa mitihani inapofanywa katika kipindi hiki cha Covid-19, waangalizi wa mitihani hii wanastahili kuwa macho zaidi.

Kutokana na sheria za kuzuia ugonjwa wa Covid-19 hasa kutogusana, wanafunzi wanaweza kutumia jambo hilo kama kinga yao kujizuia kukaguliwa, hivyo basi wafiche karatasi zenye maandishi yanayoweza kutumiwa kuibia mtihani.

Hivyo basi, tunauliza wizara ya elimu kuwajibika na kukaa macho tayari kukabiliana na visa vyovyote vile vya wizi wa mitihani.

Katika kufanya hivi, kila mwanafunzi anayefanya mtihani wa kitaifa mwaka huu atayafurahia matokeo hayo kwa kuhisi kuwa yana uwazi zaidi.

Taifa Leo inawatakia wanafunzi wote heri njema wanapoifanya mitihani yao!

You can share this post!

TAHARIRI: Wazazi wawachunge watoto na mitandao

ODONGO: Ruto agutuke awateme wanasiasa wasiomfaa