• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda vya mafua huletwa na nini?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda vya mafua huletwa na nini?

Mpendwa Daktari,

Nitakabiliana vipi na vidonda vinavyotokana na mafua kila mara, na nini kinachovisababisha?

Remmy, Mombasa

Mpendwa Remmy,

Vidonda vinavyotokana na mafua huja mfano wa malengelenge katika sehemu inayozingira mdomo na pua kila wakati unapokumbwa na mafua. Hali hii husababishwa na virusi vya Herpes simplex. Watu wengi huambukizwa virusi hivi na watoto wengine utotoni.

Virusi hivi havitoweki na badala yake vinasalia mwilini na kuchochewa ukikumbwa na msongo wa mawazo, ukiwa na mafua, au iwapo kuna mabadiliko ya kihomoni mwilini.

Hauwezi kabiliana kabisa na hali hii. Lakini unaweza kuidhibiti kwa kugogomoa mdomo kwa maji ya chumvi au dawa maalum ya kufanya hivyo; epuka vyakula au vinywaji moto; vyakula vilivyo na chumvi au viungo vingi; tumia krimu za kukabiliana na maumivu na uvimbe, na utumie dawa za kukabiliana na virusi. Kunywa maji kwa wingi na ushughulikie vyema mdomo wako.

Pia, huenda ukanufaika kutokana na vijalizo vya vitamini B na folic acid. Ikiwa vidonda hivi vitadumu kwa zaidi ya majuma mawili bila kupona, unahitaji kukaguliwa na daktari.

Mpendwa Daktari,

Juma lililopita nilishiriki tendo la ndoa bila kinga na mwanamume fulani ambaye nilikuwa nimemfahamu kwa muda wa wiki chache. Siku kadhaa baadaye nilikumbwa na mwasho katika uke wangu, ambapo baada ya kwenda hospitalini niligundulika kuwa na maradhi ya ‘Chlamydia’. Tatizo ni kwamba nimekuwa nikimhepa mume wangu kila anapotaka tushiriki tendo la ndoa kwani bado napokea matibabu. Nitaendelea vipi kufanya hivi hadi nitakapokamilisha kutumia dawa ili iwe salama kwangu na mume wangu kushiriki tena tendo la ndoa?

Lyn, Nairobi

Mpendwa Lyn,

Kugundulika kuwa na maradhi ya zinaa kunamaanisha kwamba uko katika hatari ya kukumbwa na maradhi mengine ya aina hii. Kwa hivyo litakuwa jambo la muhimu kupimwa maradhi mengine ya zinaa ikiwa ni pamoja na virusi vya HIV.

Pia, ikiwa utapatikana hauna virusi hivyo, huenda ukanufaika kutokana na dawa za kuzuia maambukizi ya HIV (Pre-exposure prophylaxis (PrEP)) ili kuzuia maambukizi ikiwa utakuwa kwenye hatari hiyo.

Huenda tayari umemuambukiza mumeo maradhi ya Chlamydia, na hivyo litakuwa jambo la busara ikiwa pia yeye atapimwa na kupokea matibabu.

Kadhalika itabidi mpimwe maradhi mengine ya zinaa hasa ikizingatiwa kwamba mara nyingi Chlamydia hayaonyeshi ishara. Hii ni muhimu pia kwani ikiwa mumeo hatopimwa na kutibiwa, kuna hatari ya kukuambukiza tena hata ikiwa utakuwa umekamilisha matibabu.

Kumbuka kwamba mbinu ya kipekee ya kushiriki tendo la ndoa na kuzuia maambukizi ni kwa kutumia kondomu vizuri.

You can share this post!

ODONGO: Ruto agutuke awateme wanasiasa wasiomfaa

KWA KIFUPI: Janga la corona limetatiza pakubwa vita dhidi...