• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 7:55 AM
NGILA: Uhuru amuige Magufuli kutumia data kuzuia wizi

NGILA: Uhuru amuige Magufuli kutumia data kuzuia wizi

Na FAUSTINE NGILA

SI mara moja au mbili ambapo aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli alitaja takwimu muhimu katika hotuba zake kwa wananchi.

Iwe ni kando ya barabara, kwenye hafla rasmi za kitaifa au alipokagua jinsi wanakandarasi walivyotekeleza miradi kwa wananchi, Dkt Magufuli angenukuu data muhimu kuhusu sekta husika.

Jumatatu, kwenye ibada ya wafu iliyofanyiwa mwili wa mwendazake jijini Dodoma, Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan alistaajabisha wengi alipowaambia waombolezaji kuwa Dkt Magufuli alikuwa anajua idadi kamili ya samaki wote katika maziwa ya Tanzania pamoja na Bahari Hindi.

Lakini mimi sikushangaa kwani tangu alipofariki, nimetazama video kadhaa katika mtandao wa YouTube kuhusu jinsi alivyokuwa ‘akitumbua majipu’ serikalini.

Niligundua kuwa katika kila mkutano wa hadhara ama wa faragha, angetaja takwimu akiwahimiza wananchi kutia bidii maishani au akiwatimua kazini maafisa wazembe au wafisadi.

Alielewa vizuri takwimu za taifa lake. Hii inamaanisha kuwa walio karibu naye walikuwa wanafanya utafiti wa kutosha kuhusu data ya uchumi wa Tanzania, Afrika Mashariki na hata bara nzima.

Ni takwimu hizi ambazo zilikuwa zinabeba ushawishi mkubwa katika hotuba zake, kwani zilikuwa za kweli, na zilichangia pakubwa kuwafungua macho Watanzania katika kipindi cha miaka mitano ambapo aliongoza taifa hilo.

Nafikiri ni kutokana na ushawishi huu wa kutumia data ya kisasa kufanya maamuzi ya kibiashara ambapo uchumi wa Tanzania ulipanuka, na hata Benki ya Dunia ikatoa ripoti Julai 2020 iliyofichua kuwa Tanzania ilikuwa imefikia Kenya kiuchumi.

Wananchi wengi nchini humo kwa sasa ni wa tabaka la chini la kati, kama tu Kenya, kulingana na ripoti hiyo.

Kwa hili Dkt Magufuli amewaachia wanasiasa wa Kenya funzo muhimu katika siasa za maendeleo. Kwa mfano, Rais wetu Bw Uhuru Kenyatta hutaja data wakati anahutubu kuhusu corona, na kupuuza data muhimu katika sekta zingine. Na wanasiasa wetu nao wamemuiga.

Unapotaja takwimu katika hotuba yako kama Rais, unachangia pakuu kuweka msingi wa kutumia data kufanya maamuzi. Rais Kenyatta anafaa kujifunza kutoka kwa Dkt Magufuli kuwa sekta zote za uchumi ni muhimu.

Iwe ni kilimo, utalii, ugatuzi, uchukuzi, mazingira, maji, ardhi, elimu, afya, mawasiliano, ujenzi, viwanda, ulinzi, mambo ya kigeni, fedha, biashara na hata michezo, takwimu muhimu zinafaa kuwa kwenye hotuba ya Rais Kenyatta kila anapoenda kukagua miradi.

Na si kutoa tu data kisha kukosa mbinu ya kuzima maovu, kila takwimu kuhusu utovu wa maadili serikalini inafaa kufuatwa na matendo ya kukomesha uovu huo.

Kwa mfano, Rais Kenyatta mapema mwaka 2021 alitaja kuwa Sh2 bilioni huibwa na maafisa wa serikali kila siku. Ni data ambayo binafsi nilifuatilia na kupata kuwa ya kweli, lakini iko wapi data ya kuonyesha mikakati ambayo serikali imeweka kuzuia wizi huu?

Rais Kenyatta alituambia kuwa Dkt Magufuli alikuwa rafiki yake lakini sasa hayupo duniani tena. Aige mbinu hiyo ya sahibu wake kutumia data kutumbua majipu kwenye serikali yake.

Asibembeleze afisa yeyote wa serikali, atumie muda wake uliosalia kuwatia ndani wanaoiba fedha serikalini kisha awape wananchi data ya maafisa aliotia adabu, mwishoni mwa muhula wake.

You can share this post!

TAHARIRI: Covid: Matumizi ya pesa yaanikwe

WASONGA: Covid: Kenya isitoe chanjo kwa wafanyakazi wa...