• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WASONGA: Covid: Kenya isitoe chanjo kwa wafanyakazi wa balozi za nchi za kigeni

WASONGA: Covid: Kenya isitoe chanjo kwa wafanyakazi wa balozi za nchi za kigeni

Na CHARLES WASONGA

MENGI ya mataifa matajiri ulimwenguni tayari yameagiza mamilioni ya dozi za chanjo ya corona kwa raia wao yakiwa mbioni kudhibiti janga hili.

Hii ndio maana kufikia sasa mataifa masikini haswa yale ya Afrika yamepokea dozi chache zaidi ya chanjo hiyo chini ya mpango wa usambazaji chanjo kwa mataifa yenye uwezo hafifu kifedha (COVAX).

Mnamo Mach 2 Kenya ilipokea dozi 1.02 milioni za chanjo aina ya AstraZeneca chini ya mpango, bila malipo. Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu ya Watoto (UNICEF) na lile la Afya Ulimwenguni (WHO) ndizo zilifadhili usafirishaji wa chanjo hiyo.

Aidha, mnamo Machi 16 Kenya ilipokea shehena nyingine ya dozi 100,000 ambayo ilikuwa msaada kutoka India.

Kwa kuwa dozi hizo ni chache, serikali iliamua kuwa wahudumu wa afya, walinda usalama, walimu na wazee na watu wenye magonjwa sugu ndio watapewa chanjo hiyo kwanza.

Lakini inashangaza kuwa sasa serikali imeamua kwenda kinyume na sera hiyo, iliyopitishwa na baraza la mawaziri, na kushirikisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa (UN) na wale wanaohudumu katika afisi za balozi za mataifa ya kigeni, katika awamu ya kwanza ya utoaji chanjo.

Kinaya ni kwamba baadhi ya mataifa hayo ya kigeni ni yale tajiri na yenye uwezo wa kununua chanjo ya Covid-19 kwa wingi.

Kwa hivyo, haiwezekani kwamba mataifa hayo hayajaweka mipango ya kuwezesha raia wao wanaohudumu katika balozi zao zilizoko mataifa ya kigeni wamepata chanjo.

Hii ni kwa sababu mataifa kama vile Amerika, Uingereza na Israeli huthamini zaidi afya na usalama wa raia wao wanaohudumu katika mataifa ya kigeni. Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba mataifa hayo yamesambaza chanjo ya corona kwa raia kama hao, wakiwemo wale wanaohudumu Kenya.

Kwa hivyo, serikali inafaa kutumia dozi chache za chanjo ya AstraZeneca ilizopokea kuwapa Wakenya wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona. Hii ni muhimu haswa wakati huu ambapo Kenya inashuhudia wimbi la tatu la maambukizi ambapo idadi ya wale wanaoambukizwa kwa siku moja ni juu zaidi.

Hospitali za humu nchini, za umma na zile za kibinafsi, zimelemewa na idadi ya wagonjwa wa corona huku idadi ya waliangamizwa na ugonjwa huu ikipita watu 2,000.

Serikali inafaa kuzingatia utaratibu wake wa awali wa utoaji chanjo katika awamu hii ya kwanza. Ikome kushirikisha wafanyakazi wa UN na balozi za mataifa ya kigeni. Mataifa hayo yashughulikie raia wao, hususan wakati huu ambapo kuna uhaba wa chanjo.

You can share this post!

NGILA: Uhuru amuige Magufuli kutumia data kuzuia wizi

GWIJI WA WIKI: Fatma Ali Mwinyi