• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
NDIVYO SIVYO: ‘Kuwa’ na ‘kua’ yana ukuruba tu wa kimatamshi, maana ni tofauti

NDIVYO SIVYO: ‘Kuwa’ na ‘kua’ yana ukuruba tu wa kimatamshi, maana ni tofauti

Na ENOCK NYARIKI

MANENO kuwa na kua yanakaribiana sana kimatamshi.

Kutokana na kukaribiana huko,si rahisi kugundua wakati yanapokosewa katika mazungumzo ya watu. Kosa kama hilo linaweza tu kubainika katika kazi andishi. Baadhi ya watumizi hushindwa kupambanua tofauti baina ya maneno hayo mawili licha ya kuwa yamejikita sana katika matumizi ya kila siku. Sababu nyingine inayochangia utata unaoyazunguka maneno hayo mawili – licha ya ile ya matamshi – ni kule kutumiwa aghalabu kwa neno ‘kuwa’ katika fasili zinazolenga ‘kua’. Kwa mfano neno furuka linaelezewa kuwa ni ‘kua mkubwa’ au ni kututumka na kuwa kubwa. Matumizi ya maneno hayo kutoa fasili tuliyoitaja, yanaingiliana mno. Aidha, njia rahisi mno ya kuelezea neno ‘kua’ ni kutumia neno ‘kuwa’. Kwa hivyo, mshikamano uliopo baina ya maneno hayo mawili unaweza kuwa chanzo kingine cha mkanganyiko uliopo.

Haitakuwa sahihi kusema kuwa utata wa kimatumizi tunaourejelea umesheheni tu shuleni. Neno hilo hukosewa pia katika vyombo vya habari na vitabu vya Kiswahili. Neno ‘kua’ ndilo aghalabu hukosewa katika matumizi. Linapotumiwa badala ya ‘kuwa’ huibua dhana nyingine tofauti sana na ile iliyodhamiriwa. Tuchukue mfano wa kauli kama hii ifuatayo: *Nimekua nikilala. Kauli yenyewe inaweza kuchukuliwa kumaanisha kuwa kitendo cha kupevuka kilikuwa kikitendeka mzungumzaji alipokuwa usingizini !

Toleo la kwanza la Kamusi ya Kiswahili Sanifu linalipa neno ‘kua’ fasili tatu kuu. Kwanza, ni kuzidi umri. Pili, ni kuongezeka kwa kimo na tatu ni kuongezeka akili; kuwa na busara.

Toleo la pili linazipunguza fasili hizo hadi mbili ambazo ni: zidi kimo kadiri umri unavyoongezeka na ongezeka akili au kuwa na busara. Maelezo hayo, japo sahihi, yamezunguka tu kiumbe – hai. Fasili ya pili ya neno hilo katika Kamusi ya Karne ya 21 – ile ya kuongezeka kwa ukubwa au kimo – inaelekea kuleta ukamilifu wa dhana yenyewe kwani kupitia kwayo dhana nyingine ya kutanuka kwa vitu ambavyo si lazima viwe na uhai inajitokeza. Kwa mfano, biashara changa zina uwezo wa kukua.

Neno kuwa – kimojawapo cha vitenzi vya silabi moja – hutumiwa kwa njia mbalimbali. Kwanza, huonyesha kutokea, kutendeka au kufanyika kwa jambo fulani. Pili, huonyesha kudumu au kubaki katika hali au mahali fulani kwa muda fulani. Mfano:Juma amekuwa kanisani akisali tangu asubuhi. Tatu, hutumiwa badala ya neno kwamba katika sentensi: Walisema kuwa watazuru shuleni kwao siku ya Jumamosi.

Ijapokuwa ‘kua’ na ‘kuwa’ yanakurubiana kimatamshi na kwamba mara nyingi hutumiwa pamoja katika tungo, ni maneno yanayotofautiana kimaana.

You can share this post!

VITUKO: Suala la chanjo kwa walimu lawa kiazi moto katika...

Mpango wangu ni kurejea Real Madrid na kufikisha usogora...