• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
JULIUS MWANZIA: Msanii chipukizi wa injili, produsa mtajika

JULIUS MWANZIA: Msanii chipukizi wa injili, produsa mtajika

Na JOHN KIMWERE

NI mwimbaji wa nyimbo za injili na produsa anayekuja kwa kasi kwenye jukwaa la muziki wa burudani. Anashikilia kuwa amepania kujituma kiume kuhakikisha amefikia upeo wa kimataifa ndani ya miaka michache ijayo.

Julius Nana Mwanzia anasema anaamini ana uwezo wa kufanya vizuri katika jukwaa la muziki wa injili. Msanii huyu kwa upande wa uimbaji anajulilkana kama J Nana ilhali kama produsa anafahamika kama Nana Break it Down.

”Ninatamani sana kuibuka kati ya waimbaji wanaotetemesha katika ulingo wa muziki wa injili duniani jambo ninalolifanyia kazi usiku na mchana,” alisema chipukizi huyu na kuongeza kuwa ingawa tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa daktari amezamia kumtumikia Mungu kupitia masuala ya muziki wa injili.

Anasema alijiunga na utunzi wa injili maana ni wito ambapo mwanzo wa ngoma alighani nyimbo iitwayo Mawimbi mwaka 2014.

Hata hivyo anadokeza kuwa alivutiwa na usanii baada ya kushauriwa na wasanii kama Benjamin Dude, Pitson kati ya wengine kuwa ana kipaji cha utunzi. Anasema kuwa katika jukwaa la muziki wa injili alitambulika mwaka 2017 baada ya kuachia fataki iitwayo ‘Mambo ya Walawi.’

Teke hiyo aliirekodi mwenyewe kwenye studio anayomiliki inayofahamika kama Hewane Records aliyoanzisha mwaka huo inayopatikana mjini Juja, Thika Road.

”Nimetunga na kutoa nyimbo nyingi tu zenye upako wa kiroho kwa kondoo wa Mungu. Ninaamini zinaendelea kuwajenga wengi huku nikitarajia kuachia zingine nyingi,” akasema. Fataki za utunzi wake zinajumuisha: ‘Mambo ya Walawi,’ ‘Mawimbi,’ ‘Siteketei,’ ‘A Million Blessings,’ ‘Bakubize,’ ‘Nisamehe,’ ‘Unanisikia,’ na ‘Neema,’ kati ya zingine.

Kama produsa, chipukizi huyu amefanikiwa kufanya kazi na wanamuziki wengi tu akiwamo ndugu yake, Isaac Mwanzia maarufu kama Zack Art aliye kati ya waimbaji wanaotamba katika muziki wa injili. Pia wapo Kenny Bizzoh, Samantha Ann, Glad Muchai, Sammy Kioko, Mwalimu Tom, Cartoon Comedian, Stephen Kasolo, Phylis Mutisya, Fari Athman, Christian Maingi na Lucinia Karrey kati ya wengine.

Chipukizi huyu anajivunia kurekodi nyimbo na kukubalika na wafuasi wengi nchini. Baadhi ya teke hizo zikiwa Loving You (Kenny Bizzoh), I feel You, Ma Feelings, Pendo for me (fataki zake Fari Athman). Pia Mzima Mzima, Kuche, Nitatangaza, Unanisikia (nyimbo zake Zack Art), Chai yangu na Sukari parody (Cartoon Comedian) na wimbo kwa jina Utawezana Parody (Sammy Kioko na Mwalimu Tom). Kama produsa anasema anapenda kutia bidii kama wenzake waliojizolea sifa tele akiwamo KrizBeats mzawa wa Nigeria na LizerClassic kati ya wengine.

Anasema anajivunia kujizolea umaarufu kiasi kwa muda mchache kwa kuzingatia mwaka uliyopita studio anayomiliki ilitwaa tuzo ya Music Brand Promoter of the Yaer (FEMA Awards). Naye binfasi kama produsa alizoa tuzo ya Audio Producer of the Year kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kenya Cinema.

You can share this post!

ANGELA CHEGE: Analenga kumpiku Anne Kansiime

FC Talent inavyokuza talanta za vijana chipukizi