GACHIE SILVER BULLETS WALENGA KUPANDA DARAJA LA PILI

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gachie Silver Bullets imepania makubwa katika soka la humu nchini lakini uhaba wa ufadhili unadidimiza azma yake. Mwenyekiti wake, Gideon Cherono anasema kuwa bila ufadhili huwa vigumu sana kwa klabu yoyote kudumisha wachezaji wazuri. Anashikilia kuwa wanataka kujituma kiume kwenye juhudi za kuwania tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

”Baada ya janga la corona kuvuruga kampeni za muhula uliyopita raundi hii tunalenga kujitahidi kadiri ya uwezo wetu ili kunasa tiketi ya kusonga mbele,” mwenyekiti huyo alisema na kuongeza kuwa ni mapema kuyeyusha matamanio yao.

Anatoa wito kwa wachezaji wake wawajibike ipasavyo viwanjani wanaposhiriki mechi za kipute hicho. Gachie Silver Bullets chini ya makocha, Solomon Shikokoti na naibu wake, Dennis Akwibasa inalenga kupigana kufa na kupona kuwinda nafasi ya kupandishwa ngazi muhula ujao.

”Tuna imani tumeanza kufanya vizuri kwenye mechi zetu msimu huu. Baada ya kucheza mechi tano tumevuna ushindi mmoja na kutoka nguvu sawa mara mbili na kuangukia pua mara mbili,” Shikokoti alisema na kuongeza kuwa wanafahamu shughuli sio rahisi maana timu zote zimejipanga kupambana mwanzo mwisho kufukuzia taji la msimu huu.

Kocha huyo anaamini kuwa wachana nyavu wake wanayo nafasi nzuri kufufua mtindo wa kushinda mechi zao kama ilivyokuwa kwenye kampeni za msimu uliyopita kabla ya kusitishwa kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona. Kocha huyo anakiri kuwa wachezaji wake wana kibarua kigumu hasa mbele ya mahasimu wakuu kama Maafande wa Nairobi Prisons, AFC Leopards Youth, Makarios 111 FC (Riruta United) kati ya timu zingine.

”Ingawa hatukumaliza mechi za ligi muhula uliyopita tulimaliza nafasi ya tano kwenye jedwali. Sina shaka kutaja kuwa itakuwa furaha kwetu endapo tutafanikiwa kufanya kweli na kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki ligi ya daraja la pili msimu ujao,” akasema. Kadhalika anadokeza kuwa katika mpango mzima anategemea huduma za chipukizi wepesi kama Samuel Okello, Dancun Siayi, Brian Njoroge (mlinda lango) na Billclinton Ndung’u.

Meneja wake, Washington Lubanga anatoa wito kwa wahisani walitokeze kusaidia klabu hiyo kwenye jitihada zao kukuza talanta za wachezaji wanaokuja. Pia anawaambia vijana wake kuwa hata mastaa wanaowinda katika michezo mbali mbali duniani walianza kama wao.

Gachie Silver Bullets inashirikisha wanasoka kama: Julius Okwaro, Cyrus Murage, Felix Ayoyi, Vishal Muhanji, Gideon Cherono (mwenyekiti), Denis Temoi, Martin Shikuku (kipa), Brian Lisabale, Samuel Okello, Hilary Okelo, Bravin Wafula (nahodha) na Felix Mukabane. Pia wapo Edwin Shiyayi, Bruce Gamina, Godfrey Nasole, Brian Bulinda, Billclinton Ndungu, Dancun Siayi na Brian Njoroge (golikipa).

Habari zinazohusiana na hii