• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Harambee Stars ilipiga Misri mara ya mwisho miaka 44 iliyopita

Harambee Stars ilipiga Misri mara ya mwisho miaka 44 iliyopita

Na GEOFFREY ANENE

MBIVU na mbichi kuhusu Harambee Stars na Pharaohs itajulikana wakati Kenya na Misri zitaumiza nyasi ugani Kasarani katika mchuano wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) leo Alhamisi usiku.

Stars ya kocha Jacob “Ghost” Mulee, ambayo itakosa nguvu za mashabiki wa nyumbani kwa sababu mashabiki hawataruhusiwa uwanjani, itakuwa ikitafuta ushindi wake wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 dhidi ya Misri.

Ili kufufua matumaini madogo inayo ya kufuzu, Stars lazima ishinde Mafirauni hao ambao iliwakaba 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza mjini Alexandria.

Mulee atawategemea sana mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020 Michael “Engineer” Olunga, ambaye wakati huu ni mchezaji wa Al Duhail nchini Qatar, Masud Juma (Difaa Hassani El Jadidi, Morocco) na mfumaji matata wa AFC Leopards Elvis Rupia kutafuta mabao.

Eric Kapaito (Kariobangi Sharks), ambaye anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Kenya, aliumia kwa hivyo atakuwa shabiki tu. Nafasi yake ilitwaliwa na winga matata Cliff Miheso (Gor Mahia) ambaye krosi zake zitahitajika zaidi leo.

Kenya imepiga Misri mara moja katika mechi 20 mataifa haya yamekutana katika historia yao. Ilichabanga Wamisri 3-1 kupitia mabao ya Aggrey Lukoye na Charles ‘Ayuke’ Ochieng (mawili). Osama Khalil alipachika bao la Misri kujiliwaza katika mchuano huo wa kufuzu kushiriki AFCON 1980 uliopigiwa katika uwanja wa City jijini Nairobi mnamo Juni 1979. Kenya ililemewa 3-0 katika mechi ya marudiano jijini Cairo na kubanduliwa.

Vijana wa Mulee walijiandaa kwa mechi ya Misri kwa kulima Sudan Kusini 1-0 (Machi 13) na Tanzania 2-1 (Machi 15) jijini Nairobi katika michuano ya kupimana nguvu.

Hata hivyo, Stars walijiweka katika hatari ya kukosa AFCON 2022 baada ya kuchapwa 2-1 ugenini na kutoka 1-1 jijini Nairobi dhidi ya Comoros mwezi Novemba 2020.

Ushindi wa Kenya leo na pia Togo ikipiga wenyeji Comoros, basi Stars itakuwa imepiga hatua muhimu ya kufuzu. Bado itahitajika kulaza Togo jijini Lome mnamo Machi 29 na kuomba mmoja kati ya Misri na Comoros ichapwe watakapokutana siku hiyo jijini Cairo.

You can share this post!

Refa mpya kwa mechi ya Harambee Stars na Misri baada ya...

Modern Coast Yazidi Kudidimia Supaligi ya Taifa