• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
TAHARIRI: Fedha: Kaunti zizingatie ushauri

TAHARIRI: Fedha: Kaunti zizingatie ushauri

KITENGO CHA UHARIRI

SERIKALI za kaunti zinastahili kuchukulia kwa uzito ushauri wa kutafuta mbinu mbadala za kupata fedha na vile vile kuzitumia kwa njia inayofaa.

Tangu utawala wa ugatuzi ulipoanza kutekelezwa baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2013, kumekuwa na mivutano mingi kati ya serikali za kaunti na serikali kuu kuhusu fedha.

Hivi sasa kuna mpango wa kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti kupitia kwa mswada wa kurekebisha katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Waasisi wa BBI wanaamini kuwa, katiba ikiagiza kwamba serikali za kaunti zitengewe kiasi kikubwa cha pesa, magavana watafanikiwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kila mara, magavana hulalamika kwamba Wizara ya Fedha inachelewa kuwatumia pesa.

Wao hudai hali hiyo ni mojawapo ya sababu zinazochangia kucheleweshwa kwa mishahara ya wafanyakazi, wakiwemo wahudumu wa afya ambao migomo yao imegeuka kuwa desturi.

Kwa upande mwingine, serikali kuu hulaumu magavana kwa kutotumia kiasi cha pesa ambacho kaunti hutengewa kwa sasa hasa pesa zinazohitajika kutumiwa katika kustawisha maendeleo.

Washauri wengi wa masuala ya kiuchumi akiwemo Mkaguzi Mkuu wa Fedha serikalini, Dkt Nancy Gathungu huwataka magavana kukaza kamba ili wajiongezee mapato bila kutegemea sana serikali kuu.

Hata hivyo, hakuna uhakika kama kiwango cha fedha kikiongezwa kwa njia yoyote ile basi matatizo ya kaunti yatatatuliwa.

Hii ni kutokana na kuwa, kando na changamoto za kupokea fedha za kutosha kwa wakati ufaao, serikali za kaunti nyingi zinatambulika kwa ubadhirifu wa fedha.

Ripoti za ukaguzi wa matumizi ya fedha kila mwaka huonyesha jinsi magavana na madiwani hutumia pesa za umma kiholela kwa mambo ambayo hayana faida kwa wananchi wa maeneo hayo.

Matumizi kama vile ulipaji mishahara kwa idadi kubwa ya wafanyakazi wasio na kazi za kufanya, au safari za kifahari kwa maafisa wa serikali, huwa ni ya kuchukiza mno.

Kando na hayo, kiwango kikubwa cha pesa pia hubainishwa kupotea kwa sakata za ufisadi.

Miongoni mwao ni zabuni zinazopeanwa kiholela ambapo kama ni za ujenzi, miradi huishia kuwa duni ilhali pesa nyingi zilitumiwa.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Bidii ya bodaboda kujikwamua kutoka kwa...

KINYUA BIN KING’ORI: UDA waache kujitanua kifua na...