• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KINYUA BIN KING’ORI: UDA waache kujitanua kifua na kuweka mikakati mipya

KINYUA BIN KING’ORI: UDA waache kujitanua kifua na kuweka mikakati mipya

Na KINYUA BIN KING’ORI

USHINDI wa mgombeaji wa chama cha Wiper kwenye uchaguzi mdogo wa useneta katika kaunti ya Machakos, dhidi ya mwaniaji wa chama kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto cha UDA unapasa kuwa funzo kubwa kwa chama hicho changa.

Licha ya mwenyekiti wa chama hicho, Johnstone Muthama kujipiga kidari na kuchukulia uchaguzi huo mdogo kama vita baina baina yake na aliyekuwa mkewe Agnes kavindu Muthama, na Chama cha wiper kinachoongozwa na kigogo wa siasa cha Ukambani, Stephen Kalonzo Musyoka, wakazi wa Machakos walimtia kidanga cha mdomo kwa kupigia mtaliki wake kura nyingi, huku mgombezi wa UDA mfanyibiashara Urban ngengele akibakia kujiuma vidole akishindwa kuamini matokeo ya kura, maana aliangushwa mwanguko wa mende kwa kujinyakulia kura 19,726 huku Kavindu akizoa kura 104, 452, na hivyo kupata asilimilia 80 ya kura hizo.

Iwapo kweli Dkt Ruto ana mipango ya kutumia chama hicho badala ya Jubilee katika azma yake ya kuwania urais 2022 anafaa ajitokeze wasiwasi na kutangazia Wakenya waelewe Ukweli wa mambo.

Chama hicho kimeshuhudia matokeo duni katika chaguzi ndogo eneo Bunge la Kabuchai na Matungu eneo la magharibi na juzi Machakos kwa sababu wanasiasa wengi Dkt Ruto anategemea kuendesha kampeni za hasla hawana umaarufu mashinani katika maeneo yao.

Siogopi kusema hawa wengine ni wale walifeli katika uchaguzi mkuu wa 2017 katika nyadhifa mbalimbali. Aidha, ni wanasiasa wanaopenda kutumia kifua, hawapendi kukosolewa wala kuzingatia ushauri wa wenzao katika kufanya maamuzi muhimu kisiasa.

Kumeibuka madai ya malumbano na mizozano katika kambi ya Tangatanga, na iwapo ni kweli, Dkt Ruto asipofanya maamuzi ya kijasiri kisiasa mapema, huenda mitego ya mahasimu wake ikamnasa na kubakia bila jeshi shupavu kisiasa kurindima ngoma yake 2022.

Kuthibitisha kambi ya Tangatanga mambo si shwari tena, Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amesusia mikutano ya kisiasa inayoandaliwa na kundi la hasla kumvumisha Dkt Ruto. Hii si dalili nzuri kwa kundi hilo na ikiwa Dkt Ruto na wapanga mikakati wake watachukulia mambo kimzaha tu watakuwa wametamauasha wafuasi wao wanaotamani awe mrithi wa Rais uhuru Kenyatta akistaafu 2022.

Matatizo ya washirika wengi wa Naibu Rais ni watu wanaomtumia kujikweza kisiasa katika maeneo yao wakilenga kujizolea umaarufu wao wakitarajia kuwa wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi wa 2022. Ndio sababu naomba Dkt Ruto kuchukua hatua ya haraka kutafuta suluhu kwa mzozo wa sasa katika cha UDA.

You can share this post!

TAHARIRI: Fedha: Kaunti zizingatie ushauri

KAMAU: Nani akomboe Kenya kutokana na ufisadi?