• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
KAMAU: Nani akomboe Kenya kutokana na ufisadi?

KAMAU: Nani akomboe Kenya kutokana na ufisadi?

Na WANDERI KAMAU

MWANDISHI mahiri, Ken Walibora aliwahi kuandika kwamba, mojawapo ya mikasa inayoiandama Afrika na nchi zenye chumi za kadri duniani, ni mtindo wa raia kuwashabikia na ‘kuwaabudu’ viongozi wao, hata wakiwa waovu.

Kwenye tamthilia ‘Mbaya Wetu’, Prof Walibora aliandika kuwa, ingawa viongozi wa kisiasa mara nyingi ndio huziingiza nchi zao kwenye matatizo yanayozikumba, raia ndio wanapaswa kulaumiwa.

Sababu kuu ni kuwa, jamii huwatetea viongozi waovu, wauaji, wezi, wachochezi, wafIsadi au hata wabakaji kwa msingi wa kuwa “mmoja wao” wala si kulingana na maadili wala utendakazi wao.

Bila shaka, ni kwa msingi huo ambapo raia hubaki kimya hata wakati viongozi ama watu wenye mienendo ya kutiliwa shaka wanapoteuliwa kuhudumu katika nyadhifa kuu na muhimu serikalini.

Hili lilidhihirika wiki iliyopita, wakati chama cha ODM kilimwidhinisha aliyekuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Umeme (EPRA), Bw Pavel Oimeke, kuwa mwaniaji ubunge katika eneo la Bonchari, Kaunti ya Kisii, kwa tiketi yake.

Uteuzi huo ulifanywa licha ya Bw Oimeke kuondolewa ofisini kutokana na sakata kadhaa za ufisadi anazohusishwa nazo.

Kama kwamba hilo halitoshi, serikali iliidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Seneta wa Murang’a, Bw Kembi Gitura, kama mwanachama wa bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA). Vile vile, uteuzi huo ulifanywa licha ya Bw Gitura kukabiliwa na tuhuma za ufisadi kufuatia sakata ya uporaji wa mabilioni ya pesa katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa Kenya (KEMSA).

Hadi sasa, Bw Gitura ndiye mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Kuna uwezekano wizi na uporaji unaofanyika katika taasisi mbalimbali serikalini huwa “maagizo” ya watu fulani wenye ushawishi? Je, wanaoteuliwa huwa wanapewa majukumu hayo kimakusudi kusimamia wizi? Kuna uwezekano teuzi zao kwenye taasisi nyingine ni “thawabu” za kusimamia vizuri wizi kufanyika?

Kwenye kitabu ‘Ninteen Eighty Four’ (1984), mwandishi George Orwell asema kuna uwezekano katika siku za usoni, huenda sote tukaishi katika mazingira ambako wizi, uporaji, mauaji, uchochezi kati ya maovu yale yote mengine yatakuwa sehemu ya maisha inayokubalika. Maadili yatakuwa ujinga na maisha yasiyokubalika.

Je, tushafika kiwango hicho? Ikiwa hali ni hiyo, ni nani atanusuru kizazi hiki na kukirejesha katika njia ifaayo kimaisha?

Imani yangu ni kuwa, kwa kutathmini upya mwelekeo wake kisiasa, kiuchumi na kijamii, kizazi hiki kina uwezo kujikomboa tena kutoka mgogoro wa kimaadili unaokikumba kwa sasa.

Kuna mifano ya nchi nyingi ambazo zimejikomboa kutoka kwa minyororo ya viongozi wasiojali, baada ya kugundua makosa yake.

Baadhi ya nchi hizo ni Burkina Faso katika miaka ya themanini, kupitia mwanamageuzi Thomas Sankara.

Kabla ya kusombwa na wimbi la mapinduzi ya kijeshi na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, DR Congo pia ilikuwa imepata mwanga wa ukombozi kwa viongozi kama Patrice Lumumba, aliyehudumu kama waziri mkuu wake wa kwanza.

Je, nani atakayejitokeza kukikomboa kizazi cha sasa?

[email protected]

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: UDA waache kujitanua kifua na...

BETWAY CUP: Congo Boys wangali wataka kucheza na Gor uwanja...