• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
SGR ya Kisumu kukamilika 2022

SGR ya Kisumu kukamilika 2022

NA RICHARD MAOSI

WAZIRI wa Uchukuzi James Macharia siku ya Jumanne aliongoza zoezi la kukagua, awam ya pili ya Reli ya Kisasa(SGR) kutoka Longonot mpaka Naivasha..

Macharia aliandamana na Waziri wa Utalii Najib Balala, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Betty Maina ambaye anasimamia viwanda.

Macharia alisema reli ya SGR, itaunganisha Longonot na Naivasha na hatimaye kaunti ya Nakuru, Malaba na Kisumu kufikia mwaka ujao 2022.

Kulingana naye mradi huu utasaidia kusafirisha shehena ya mizigo kutoka Bandari ya Mombasa hadi Malaba kwa siku mbili, jambo ambalo litasaidia kupunguza msongamano wa malori barabarani na kuhakikisha kuwa bidhaa zinafika kwa wakati zikiwa salama.

Aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa mradi wa kutengeneza SGR umefikia hatua muhimu, ikizingatiwa kuwa awamu ya kwanza kutoka bandarini Mombasa mpaka Maai Mahiu imekamilika.

“Shughuli ya kukarabati reli ya zamani na kuibadilisha iwe ya kisasa imeanza mara moja.Tunalenga kuunganisha Longonot , Naivasha, Malaba na Kisumu,”akasema.

Mkandarasi aliyepatiwa jukumu la kutengeneza reli ya SGR alipatiwa muda wa mwaka mmoja kukamilisha ukarabati, lakini inaonekana atakamilisha miezi mitatu kabla ya muda uliotolewa.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia,Waziri wa Utalii Najib Balala, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Betty Maina ambaye anasimamia viwanda, wakiwa katika eneo la Maai Mahiu kukagua reli mpya ya SGR siku ya Jumanne.

Macharia alisisitiza kuwa mpangilio mzuri wa serikali ndio umeharakisha mambo, huku akiwahakikishia raia, nafasi nyingi za ajira pindi mradi utakapokamilika.

Kwa upande mwingine Waziri wa Ugatuzi Eugiene Wamalwa alisema SGR itafikia maeneo ambayo yalihisi kuwa yanatengwa na mpango huu wa serikali.

“Kwa mfano Kitale ilikuwa ikijulikana kama mwisho wa reli lakini sasa wakazi watafurahia huduma bora za kisasa kutokana na mradi mpya, hii ni baada ya shughuli za uchukuzi wa reli kukwama mara tu baada ya Shirika la Reli kuanguka,”aliongezea.

Najib Balala alimuunga mkono akisema ameridhika kwa kazi ambayo imefanyika ambapo mwezi wa tisa itakuwa sikukuu kubwa, maana hiyo reli itafika Malaba na ifikapo mwezi wa tatu mwaka ujao itakuwa Kisumu.

“Hapatakuwa na hali ya kupoteza wakati mwingi maana shehena zitachukua muda mfupi kutoka Bandari ya Mombasa mpaka Malaba,”akasema.

Aliongezea kuwa tayari Reli ya kisasa imesaidia mambo ya Utalii kule Voi na maeneo ya Taita Taveta, Emali na Amboseli.

Itakuwa ni rahisi kutembelea mbuga ya wanyama ya Maasai Mara, na ndio maana wageni kutoka Nairobi wanaweza kutembelea maeneo ya Longonot na Hells Gate kwa siku moja na kurejea.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Wabunge wanaodaiwa kupokea hela za mafuta...

Maafisa wa kaunti motoni kwa kupatikana na silaha