• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Diwani ajitenga na ufadhili wa ghasia Kapedo

Diwani ajitenga na ufadhili wa ghasia Kapedo

 NA RICHARD MAOSI

Nelson Lotela ambaye ni mwakilishi wadi wa Silale, kutoka kaunti ya Baringo amejitenga na madai kuwa amekuwa akichochea vita vinavyoshuhudiwa eneo la Kapedo.

Akizungumza katika makao ya Director Of Criminal Investigations DCI kaunti ya Nakuru siku ya Alhamisi , aliomba serikali kuharakisha operesheni ya kuleta utulivu Kepedo.

Kulingana naye haelewi mbona jina lake limekuwa likitajwa kila mara majangili wanapovamia watu na kuiba mifugo.

“Polisi wamekuwa wakiniandama kwa madai ambayo sio kweli, ilhali kuna viongozi wengine ambao wanaweza kupanga mashambulizi,”akasema.

Aidha Lotela alieleza kuwa Silale inapatikana mbali sana na Kapedo, sehemu ambayo imekuwa ikikumbwa na mizozo ya kila wakati.

Lotela aliambia Taifa Leo dijitali hakuwa na habari kuhusu mikutano ya kupanga namna ya kuwashambulia polisi Kapedo.

“Serikali inaweza kushirikiana na wakazi wa Baringo kurejesha hali ya amani na utulivu badala ya kulenga watu wachache wasiokuwa na hatia,”alisema.

Lotela aliandikisha taarifa na DCI na hatimaye kuzungumza na wanahabari, ambapo alidai kuwa eneo la Kapedo limejaa wahalifu ingawa hakuwa akishirikiana nao.

Mara ya kwanza Lotela alijisalimisha kwa polisi siku ya Jumamosi, baada ya mshirikishi wa Bonde la Ufa George Natembeya kutoa amri ya viongozi wa Baringo kuchunguzwa.

Kulingana na Natembeya mwakilishi wadi huyo pamoja na mbunge wa Tiaty William Kamket ni baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa, na huenda wamekuwa wakishirikiana na majangili..

Hili linajiri baada ya waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’ kudai kuwa serikali inaendeleza uchunguzi ili kubaini wanaochangia mauaji katika eneo la Kapedo, Tiaty na Arabai.

You can share this post!

Jinsi serikali inavyozima kampeni ya wilibaro ya Ruto

Biden, Uhuru washauriana kuhusu ushirikiano