• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
CORONA: Uwezo wa chanjo ya China katika kuisaidia Afrika kukabili upungufu

CORONA: Uwezo wa chanjo ya China katika kuisaidia Afrika kukabili upungufu

Na MASHIRIKA

MNAMO Machi 2021, Kituo cha Kupambana na Maradhi barani Afrika (Afrika CDC), kilitangaza kuwa bara hili bado linakabiliwa na changamoto ya kupata chanjo ya Covid-19.

Afrika inapanga kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya watu wake ili kuthibiti msambao wa maambukizi ya virusi hivyo.

Likiwa na zaidi ya watu bilioni moja na chini ya chanjo milioni nne tu hadi sasa, ni dhahiri kuwa bara la Afrika litakuwa na ugumu wa kufikisha chanjo kwa watu wengi ndani ya muda mfupi.

Ulafi wa nchi za Magharibi

Ikiwa wazi kwamba nchi za Afrika hazina uwezo wa kisayansi wa kuzalisha chanjo, shirika liliso la kiserikali la The People’s Vaccine Alliance, linaripoti kuwa nchi tajiri zaidi zinazowakilisha asilimia 14 tu ya watu wote duniani zimenunua zaidi ya nusu ya chanjo za Covid-19.

Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa chanjo milioni 460 zimetolewa lakini Afrika imepokea chini ya asilimia mbili tu licha ya kuwa na asilimia 18 ya watu kote duniani.

Afrika ilifanya uagizaji wa awali wa dozi milioni 900. Lakini Afrika CDC imesema inahitaji angalau dozi bilioni 1.5 ili kuwachanja asilimia 60 ya watu.

Mchakato wote wa kununua na kugawa chanjo hizo huenda ukagharimu hadi Dola milioni 10 ambazo ni sawa na Sh1 bilioni.

Ikiwa tayari nchi za Magahribi zimenunua dozi nyingi za chanjo na kukosa kutoa misaada kwa nchi maskini, ni wazi kwamba Afrika haiwezi kutegemea nchi hizo.

Wakati uo huo, pia sauti za kutilia shaka usafirishaji wa chanjo za kampuni kama vile Pfizer hadi Afrika zinaendelea kuongezeka.

“Chanjo hizi hazikutengenezwa kwa ajili ya matumizi katika nchi zinazoendelea. Lazima zigandishwe”, anasema mwanzilishi wa jukwaa la habari la China-Afrika, Eric Olander.

“Chanjo hizi hazina faida kwa nchi nyingi zinazoendelea kwa sababu miundo-mbinu ya kuzihifadhi haipo,” anaeleza Olander.

Kwa upande mwingine, China inasisitiza kuwa chanjo zake zinaweza kuhifadhiwa kwa urahisi kwenye jokofu la kawaida tu.

China yaziba mwanya wa chanjo Afrika

Kwa kuzingatia kasi ya sasa ya utoaji wa misaada ya chanjo ya China, kuna matumaini ya kufanikisha kasi ya kuwafikia watu wengi barani humo.

Tayari China imepeleka msaada wa chanjo ya Covid-19 katika nchi za Gabon, Zimbabwe, Namibia, Djibouti, Niger, Benin miongoni mwa nyingine.

Mnamo Februari, China ilitangaza kuwa itatoa chanjo ya Covid-19 kwa nchi 19 za Afrika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni nchini China, Wang Wenbin anasema China pia inasaidia kampuni zinazouza chanjo katika nchi za Afrika na ambako zinahitajika zaidi.

Hadi kufikia sasa, China ndiyo nchi ya kwanza miongoni mwa mataifa makubwa zaidi duniani kuanza kutoa misaada ya chanjo kwa Afrika.

Mapema mwezi Mei, Rais wa China, Xi Jinping, aliahidi kuwezesha chanjo za Covid-19 zipatikane hasa kwa nchi za Kanda ya Kusini mwa dunia; yaani Global South.

Lakini si chanjo tu, China pia ilikuwa ya kwanza kutuma vifaa vya kupamba na corona Afrika pindi janga hili liliporipotiwa katika baadhi ya mataifa ya bara hilo.

Msomi na mtaalamu wa masuala ya China na Afrika nchini Kenya, Stephen Ndegwa, anapongeza mchango wa China katika hatua muhimu inayoendelea sasa hivi ya utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Anasema China imekuwa msitari wa mbele kushirikiana na nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Afrika, na kutoa msaada wa kiufundi na wa vifaa.

Bila shaka nchi za Magharibi zitaendelea kukosoa ushirikiano mpya wa China na Afrika katika suala la kukabiliana na janga la corona.

Lakini kashfa kama hizo zimeendelea kukosolewa kwa misingi ya ukweli na hali halisi.

Aliyekuwa Waziri wa Afya nchini Rwanda, Agnes Binagwaho, anaona kuwa kujali kwanza afya ya wananchi ni kupaumbele.

Anasema, “Ikiwa China itafanikiwa kutoa chanjo na kuokoa maisha ya Waafrika wengi, unadhani kwamba watu barani humo wataichukia China?”

Ufanisi wa chanjo ya China

Hadi sasa, viongozi kadhaa duniani na watu waliopata chanjo ya Sinovac kutoka China hawajalalamikia madhara yoyote kutokana na chanjo hiyo.

Japo kwa kawaida, ufanisi na usalama ni viashiria vikuu vinavyotumiwa kutathmini ubora wa chanjo; lakini siku zote usalama ni kipaumbele.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani, kati ya watu milioni mbili waliopata dozi ya kwanza ya chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer nchini humo, watu 4,000 walionyesha dalili za madhara yake makubwa.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa mamlaka ya dawa ya Norway imesema watu zaidi ya 30 nchini humo wameaga dunia baada ya kupata chanjo ya Pfizer. Kinyume na waliopata chanjo za China, kati ya watu milioni 15 kutoka nchi 125, hakuna hata mmoja aliyefariki au kuugua kiasi cha kufikia hali mahututi, wala kuonyesha madhara makubwa.

Kuhusu ufanisi wa chanjo za China, takwimu zilizotolewa na nchi mbalimbali zimeonyesha kuwa na asilimia 50 hadi 90, kiasi ambacho ni juu ya kiwango cha chini cha ufanisi wa chanjo kinachokubaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wingi wa watu na nidhamu ya China

China ikiwa ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, inasukumwa na jukumu la kuzalisha chanjo nyingi ili kufikia watu wote nchini humo.

Lakini pia haiwezekani kabisa kutegemea chanjo kwa asilimia 100 katika vita dhidi ya corona, hivyo nidhamu na kufuata maagizo ya mamlaka husika nchini humo zimekuwa nguzo muhimu katika kupunguza maambukizi.

Kufikia sasa, maambukuzi yanayopatikana nchini humo ni kutokana na watu wanaoingia kutoka nje, wala si wale walioko China tayari.

You can share this post!

KCSE: Waziri aonya wanafunzi wa vyuo

KTDA yabishana na Rais kuhusu chaguzi za wakuu viwandani