• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
MATHEKA: Wimbi la tatu la corona lachangiwa zaidi na viongozi

MATHEKA: Wimbi la tatu la corona lachangiwa zaidi na viongozi

Na BENSON MATHEKA

WIMBI la tatu la virusi vya corona nchini linalotishia nchi lingeepukwa iwapo viongozi wangeonyesha Wakenya mfano mwema.

Viongozi wakiwemo wa kisiasa, wa kidini na maafisa wa serikali walipuuza na wanaendelea kupuuza kanuni za wizara za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Wanasiasa walipokuwa wakiandaa mikutano mikubwa ya kisiasa, viongozi wa kidini nao waliruhusu waumini kujazana katika makanisa na misikiti bila kuvaa barakoa na kudumisha umbali. Maafisa wa serikali walipokuwa wakiruhusu halaiki kuhudhuria mazishi, wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma na wamiliki wa vilabu walikubali abiria na wateja kujazana katika matatu na maeneo ya burudani.

Inasikitisha kuona kuwa hata baada ya nchi kukumbwa na wimbi la tatu la maambukizi ya virusi hivi, kanuni za wizara ya afya zinaendelea kupuuzwa.

Taarifa ambazo waziri wa afya Mutahi Kagwe, wataalamu wa afya na Baraza la Maabadi wamekuwa wakitoa kusisitizia umma umuhimu wa kuzingatia kanuni hizi imekuwa sawa na kupigia mbuzi gitaa.

Licha ya wataalamu kuonya wimbi hili ni hatari na kwamba hospitali zinalemewa na ongezeko la wagonwa, kuna Wakenya wanaoamini kwamba serikali inabuni idadi ya maambukizi na vifo. Wanamini kuwa serikali inataka kuweka mazingira ya kuiwezesha kupata misaada ya kifedha kutoka mashirika wafadhili. Baadhi yao wanasema haiwezekani maambukizi ya virusi hivyo kuwa yanaongezeka nchini ilhali maafisa wa serikali wanakiuka kanuni za wizara ya afya. Kuna wanaohisi kwamba serikali inataka kupata pesa za kupora ilivyofanyika katika sakata ya mabilioni ya pesa za kushughulikia janga hili mwaka jana.

Haya yote yamechangiwa na viongozi na maafisa wa serikali kwa kutokuwa msitari wa mbele kuzingatia kanuni za afya kiasi cha kuchelewesha vitanda vya hospitali ilivyonunua mwaka jana kutoka kwa mafundi wa humu nchini.

Ni wazi kuwa licha ya wataalamu kuonya kwamba kushuka kwa maambukizi Disemba na Januari Kenya haikuwa imeangamiza virusi hivyo, serikali za kaunti na ya kitaifa zililegeza juhudi za kuzuia msambao wa corona hadi zikagutushwa na wimbi hili la tatu.

Ni kweli, serikali haina polisi wa kusimamia Wakenya wote wafuate kanuni za afya ya umma lakini viongozi wana jukumu la kuonyesha uongozi bora kwa vitendo.

Inasikitisha kufikia sasa, wanasiasa, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali wanatoa maagizo ambayo hawatimizi. Hii itazidisha hatari ya maambukizi ya corona raia wakiwaiga.

You can share this post!

Scotland na Austria nguvu sawa katika mchuano wa kufuzu kwa...

KAMAU: Raia wasihangaishwe sababu ya maendeleo