• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
Covid: Wanaohepa chanjo kuadhibiwa

Covid: Wanaohepa chanjo kuadhibiwa

Na OSCAR KAKAI

GAVANA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo ametishia kuwafuta kazi maafisa wa kaunti ambao hawatajitokeza kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Hii ni licha ya kuwa, serikali ilitangaza upokeaji chanjo ni kwa hiari ya mtu.

Kiongozi huyo ambaye jana alipokea dozi yake ya kwanza ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kapenguria, aliwataka watu wote ambao wana uwezo waende kupokea chanjo hiyo.

Prof Lonyangapuo alisema ni aibu kwa wafanyikazi wa kaunti kukosa kupokea chanjo hiyo ilhali wanafaa kuwa mstari wa mbele kuongoza kwa mfano.

“Hatutaki aibu. Hatutakuwa na mshahara kwa afisa ambaye hatapokea chanjo. Ninaomba maafisa wote wa kaunti kuongoza kwa mfano kwa kuhakikisha kuwa wanachanjwa. Wale ambao hawatashiriki kwenye zoezi hili na wako kwenye serikali yangu watakuwa wanaonyesha mfano mbaya kwa umma,” alisema.

Kulingana na mwongozo kutoka kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kuna watu ambao hawastahili kupewa chanjo kama vile, wanaopata matatizo ya kiafya wanapotumia aina fulani za dawa.

Prof Lonyangapuo alipuuzilia mbali uvumi na uongo ambao unaoenezwa kuhusu chanjo hiyo akisisitiza kuwa ni salama kwa afya ya binadamu.

Aliwataka wakazi wote wa kaunti ya Pokot Magharibi kuendelea kufuata maagizo ya wizara ya afya huku serikali ikiendelea kupambana na janga hilo.

“Tunataka wahudumu wa afya kupokea chanjo sababu ni salama na imeidhinishwa,” alisema.

Prof Lonyangapuo aliutaka umma kukoma kusikiza uongo kuhusu chanjo hiyo na kujitokeza kwa wingi kuchanjwa.

“Ninaomba wakazi wote wa hapa na wakenya kwa ujumla bila uoga sababu chanjo hiyo itasaidia kuzuia ugonjwa wa corona kupunguza maambukizi,” alisema.

Gavana huyo aliwatahadharisha wale ambao wanaeneza uvumi kuhusu chanjo hiyo akisema kuwa hakuna serikali ambayo inaweza kuidhinisha chanjo ambayo ni hatari kwa raia wake.

Hata hivyo, gavana huyo ambaye alipokea chanjo hiyo kwa kielelezo aliwataka viongozi wengine kujitokeza na kuwa msitari wa mbele kuchanjwa.

“Wakenya wanafaa kukoma kushuku chanjo sababu kuwa viongozi bado hawajachanjwa na kudai kuwa kuna kitu wanajua,”alisema.

Afisa wa matibabu katika hospitali ya Kapenguria Dkt David Karori alisema kuwa kaunti hiyo imechanja wahudumu wa afya 216 ambapo 166 ni wa kiume na 50 ni wanawake kati ya 1,500.

Daktari huyo ambaye alijiunga na gavana kuwahimiza wakazi na wafanyikazi wa serikali kuchanjwa na kuendelea na kufuata maagizo ya kuzuia ugonjwa wa corona.

Kaunti ya Pokot Magharibi imepokea dosi 6,000 za chanjo ambayo inalenga wahudumu wa afya ambao wako msitari wa mbele.

You can share this post!

Wakenya waendea medali za dhahabu ndondi za Ukanda wa Tatu...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Waislamu walinde umoja, undugu...