Azirai mke kufichua ana sponsa

Na TOBBIE WEKESA

KIMBO, Ruiru

LOFA mkazi wa hapa alipigwa na butwaa baada ya mke wake kufichua kwamba amekuwa akilishwa na mpango wake wa kando.

Inasemekana kila siku kipusa akirejea nyumbani kutoka kazini, hakukosa kilo moja ya nyama ya mbuzi ama nguruwe mkobani ambao jamaa alikuwa akifurahia.

Penyenye zinasema polo na mkewe walikuwa wakizozana kila mara. Mwanadada alikuwa akimuonya polo kukoma kukimbiakimbia kwa mamake kuomba usaidizi badala yake atafute kazi ya kufanya ili akidhi mahitaji ya familia yake.

Inasemekana mwanadada aliamua kumfichulia polo siri baada ya kuudhika na tabia yake.

“Wewe ni mwanamume sampuli gani. Kila saa uko kwa mama yako. Kwani utalishwa hadi lini na wahisani,” mwanadada alimfokea polo.

Inadaiwa polo alibaki mdomo wazi asielewe alichoamanisha mkewe.

“Tangu huu mwezi uanze umekuwa ukirarua nyama ya mbuzi bila huruma. Kwani unafikiria huwa ninaitoa wapi?” kidosho alimuuliza polo.

Duru zinasema polo aliamua kuondoka akifikiria mkewe alikuwa na nia ya kumdhalilisha.

“Hata ukienda. Kuanzia leo jua ya kwamba mpango wangu wa kando hataendelea kukulisha,” mkewe alimuonya polo.

Polo aliposikia tamko la mkewe, mate yalimkauka kinywani.

“Ile siku mtu wangu atakoma kununua chakula ndio utajua maisha ni magumu. Endelea kukimbiakimbia kwa mama yako tu badala ya kutafuta kazi kama wanaume wengine,” mkewe alimzomea polo.

Duru zinasema polo alishindwa la kufanya. Alitamani ardhi ipasuke na immeze mzimamzima.

Habari zilizotufikia zinasema alipandwa na hasira na kutaka kumzaba mkewe makofi lakini mwanadada aligundua njama ya polo na kuchomoka mbio.