• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
TAHARIRI: Kufungwa kaunti 5 kutaumiza wengi

TAHARIRI: Kufungwa kaunti 5 kutaumiza wengi

KITENGO CHA UHARIRI

HATUA ya serikali ya kufunga kaunti tano zilizolemewa na maambukizi ya virusi vya corona bila shaka itaathiri Wakenya wengi na kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Ni hatua ambayo haikutarajiwa na wengi ikizingatiwa kuwa hali ya kawaida ya kiuchumi ilikuwa imeanza kurejea nchini miezi mitatu tu baada ya masharti ya kuzuia msambao wa virusi hivyo yaliyotangazwa mwaka jana kulegezwa.

Hakuna shaka kwamba virusi hivyo ni hatari na kusema kwamba Wakenya wengi wakiwemo viongozi walikuwa wamepuuza kanuni za wizara ya afya hadi wimbi la tatu lilipothibitishwa nchini sio jambo la kubisha.

Kulingana na serikali, haikuwa na budi kufunga kaunti hizo tano ili kuokoa maisha ya Wakenya. Lengo la kuchagua kaunti hizo tano ambazo ni kitovu cha uchumi wa nchi ni kuzuia watu kusafiri hadi kaunti nyingine 42 na kusambaza virusi.

Hii sio hatua mbaya. Hata hivyo, serikali ilifaa kuweka mipango ya kukinga wakazi wa kaunti hizo na athari watakazosababishiwa na marufuku iliyoweka.

Mwaka jana, kanuni za kukabiliana na janga hili zilisababisha janga jingine la kiuchumi kuporomoka na kufanya mamilioni ya watu kupoteza kazi na hadi wakati huu wangali wanateseka.

Hali ilikuwa mbaya hivi kwamba dhuluma za nyumbani ziliongezeka baada ya watu kusongwa na mawazo kwa kukosa mbinu za kujipatia mapato.

Kwa kuwa marufuku ya sasa yanadumu kwa muda usiojulikana ikiwemo kufungwa kwa shule, uchumi wa kaunti hizo tano bila shaka utaathirika pakubwa.

Pengine serikali inaweza kufikiria kusitisha mpango wa Kazi Mtaani katika kaunti nyingine na kuongeza idadi ya wanaonufaika kaunti tano ilizofunga ili kuwakinga wakazi wanaokabiliwa na hali ngumu.

Hivyo basi, itabidi wakazi wa kaunti hizo kuzingatia kwa makini kauni za wizara ya afya ili maambukizi yaweze kupungua kwa muda mfupi yafunguliwe wakazi waendelee na shughuli zao za kawaida.

Hii itawezekana iwapo wakazi hawatatumia ujanja waliozoea kukiuka kanuni zilizowekwa kuthibiti maambukizi.

Zikiwa kitovu cha uchumi wa nchi na kanda nzima ya Afrika Mashariki, athari za kufungwa kwa kaunti hizo zitafika kaunti nyingine zote 42 na nje ya mipaka ya Kenya.

You can share this post!

Azirai mke kufichua ana sponsa

JAMVI: Suluhu atarudisha urafiki na majirani?