• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
TANZIA: Mama Sarah Obama afariki

TANZIA: Mama Sarah Obama afariki

Na SAMMY WAWERU

NYANYA ya aliyekuwa Rais wa Amerika, Bw Barrack Obama, Mama Sarah Obama amefariki. Mama Sarah, ambaye alikuwa mjane, mke wa tatu wa babu ya Rais Obama amefariki dunia mapema Jumatatu.

Binti yake yake, Marsat Obama ametangaza Mama Sarah alifariki katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga, Kisumu, ambapo alikuwa anapokea matibabu.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa alilazwa humo Jumapili asubuhi.

Huku taifa na ulimwengu ukimuomboleza, Mama Sarah na ambaye ni Mkenya, atakumbukwa kutokana na jitihada zake kupiga jeki sekta ya elimu.

Alikuwa ‘mwalimu’ na mfadhili wa Wakfu wa Masomo wa Mama Sarah (Foundation), uliolenga kutoa ufadhili wa karo na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi kwa wanafunzi wasiojiweza katika jamii.

Mradi huo ukiwa eneo la Kogelo, Kaunti ya Siaya, anakotoka,umekuwa wa manufaa makubwa kwa mayatima na familia zisizojiweza kwa kuwapa lishe, mavazi na kuwalipia karo.

“Kama taifa tumempoteza kiungo muhimu katika sekta ya elimu na jamii. Ni mama mkarimu kutokana na matendo yake, na niliyepata fursa ya kutangamana naye ana kwa ana,” akasema Bw Wilson Sossion, mbunge maalum na Katibu Mkuu wa KNUT, akituma salamu za pole kwa jamaa, marafiki na taifa kwa jumla.

Kutokana na jitihada zake katika jamii, Mama Sarah Obama amepokea tuzo mbalimbali nchini na pia katika ngazi ya kimataifa.

Rais Obama alipotembelea Kenya mara ya mwisho mwaka wa 2018, alizuru Kogelo na kutangamana na nyanya yake.

Akiwa mamlakani, pia alizuru Kenya 2015.

Mwaka wa 2014, Mama Sarah alifanya ziara Amerika kutafuta wafadhili na kuchangisha fedha za Wakfu wake.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 99, na kulingana na mmoja wa wanafamilia maandalizi ya mazishi kumpumzisha leo yanaendelea.

You can share this post!

Afrika yalia Ulaya, hasa Ufaransa ‘inaiba’...

Mamia ya wasichana wafanyia KCSE hospitali baada ya...