• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
Jambazi sugu Maragua aponea kuuawa na polisi baada ya kufumaniwa akilisha makurutu kiapo

Jambazi sugu Maragua aponea kuuawa na polisi baada ya kufumaniwa akilisha makurutu kiapo

NA MWANGI MUIRURI

Kinara wa genge la uvamizi wa mauaji katika Kaunti ya Murang’a ameponyoka mauti baada ya kuponea chupuchupu alipokoswa na risasi ambayo alikuwa amelengwa na maafisa wa polisi alipofumaniwa akilisha vijana watatu kiapo kwa mto.

Genge linalodaiwa kuwa lake linafahamika kama Jeshi ya Gaica ambalo huwa na ngome yake katika Kijiji cha Maica Ma Thi Kilichoko Kaunti ndogo ya Maragua.

“Hili ndilo genge ambalo limekuwa likitutatiza katika eneo hilo ambapo limehusishwa na kuvamia raia na kuwajeruhi vibaya kiasi cha baadhi yao kupoteza uhai wao,” akasema mkuu wa Polisi wa Murang’a Kusini, Bw Anthony Keter.

Alisema kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria katika Kijiji hicho walipata dokezi kuwa Mshukiwa huyo kwa jina John Mburu Maina alikuwa katika kingo za Mto akiwa katika hafla ya kulisha kiapo wafuasi watatu wapya wa umri wa ujana katika genge lake.

“Wafuasi hao hulishwa kiapo cha ujasiri, uaminifu na pia cha ukakamavu wa mapambano dhidi ya polisi, machifu na raia ambao watajaribu kuvamia biashara yao ya upishi na uuzaji Chang’aa na mauzo ya bhangi ili kupata ufathili wa harakati zao,” akasema.

Bw Keter alisema kuwa baada ya maafisa hao kumkabili mshukiwa na kumwamurisha ajisalimishe, alitwaa mishale aliyokuwa nayo na akalenga shabaha akiwa na nia ya kuvamia maafisa hao.

“Ndipo alilengwa kwa bunduki na risasi moja ikafyatuliwa, ikamkosa kwa karibu na ndipo alitoroka akiwaacha makurutu wake waliokamatwa. Kulikuwa na lita 20 za pombe ya Chang’aa ambayo baada ya kulishwa kiapo, watatu hao walikuwa wakaiuze kwa niaba ya genge la mshukiwa,” akasema.

Kibango cha kuelekeza hadi kituo cha polisi cha Maragua. Picha/ Mwangi Muiruri

Aidha, kulipatikana nyama na damu ya mnyama usiotambulika ambazo zilikuwa zikitumika katika kiapo hicho.

Bw Keter alisema kwamba maafisa hao walifika katika Nyumba ya mshukiwa na ambapo waliipekua na kutwaa silaha butu zinazoaminika hutumika katika uvamizi wa genge hilo.

Awali, maafisa hao walikuwa wamenasa bhangi na chang’aa ndani ya baa moja ya eneo hilo huku nao wengine wawili waliokuwa wakisakwa kwa kina kwa kuhusishwa na mauzo ya mihadarati katika Shule ya Upili ya eneo hilo wakikamatwa.

Maafisa hao wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Maragua Bw Cleophas Mangut Juma na Mkuu wa Tarafa ya Ichagaki Bw Joshua Okello walivamia baa moja inayofahamika kama Prime Bar iliyoko katika mtaa wa Ichagaki ambapo habari za ujasusi zilikuwa zimebainisha kuwa ilikuwa imefurika wateja mwendo wa saa moja asubuhi.

Ni hapo ndani ambapo kulinaswa gramu 800 za bangi zikiwa na mshukiwa wa kiume ambaye wiki jana aliponyoka mtego wa polisi baada ya kuripotiwa alikuwa amepatikana karibu na Shule ya Upili ya Wavulana ya Ichagaki akiuzia wanafunzi mihadarati.

“Tulimfumania na baada ya kumkamata, akaponyoka na akafanikiwa kuhepa. Lakini Jumapili asubuhi tukampata tena akiwa ndani ya baa hiyo akishirikisha biashara yake. Yuko ndani sasa na hana nafasi ya kutoroka,” akasema Bw Okello.

Maafisa wa polisi walisema kuwa mlanguzi huyo anayefahamika kama John Kihoro Wainaina na ambaye pia alikuwa amenaswa na kilo 50 za bhangi hivi majuzi katika mtaa wa Sabasaba lakini kesi yake ikazama kwa njia isiyoeleweka ni mwiba sugu katika vita dhidi ya mihadarati eneo hilo.

Wakikamatwa, kulizuka mshikemshike wakati washukiwa waliokuwa ndani ya baa hiyo walivunja mlango wakiwa na nia ya kushambulia maafisa hao ndio watoroke lakini wenyeji wakaingilia kati na kupiga jeki juhudi za maafisa hao za kuwathibiti.

“Kunao walikuwa na mapanga na ambao ni vijana wa kulinda biashara haramu za pombe na mihadarati eneo hili. Kwa kuwa mwenye baa alikuwa amekataa kufungua mlango akiwataka watulie ndani, wakati maafisa wa polisi walipotisha kurusha mikebe ya vitoa machozi ndani ya baa hiyo ndipo genge hilo liliazimia kuvunja mlango,” akasema shahidi James Karanja.

Aidha, kuna wengine ambao walijaribu kutorokea kwa paa la baa hiyo huku katika harakati hizo wakiharibu siling’i na mabati.

Bw Okello alisema kuwa kando na Bw Wainaina, kulinaswa mlanguzi mwingine aliyetambulika kama Stephen Njoroge Kimani ambaye alikuwa na vifurushi 13 vya bhangi iliyokuwa imesagwa tayari kufungwa iwe misokoto.

“Cha ajabu kuu ni kwamba, huku leseni ya baa hiyo inayomilikiwa na Bw Julius Kinuthia Wanyoike ikimpa idhini tu ya kuuza pombe zinazofahamika na vitengo vya serikali, alikuwa na lita 58 za Chang’aa na ambazo alikuwa akiuza,” akasema Bw Okello.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Bw Anthony Keter, washukiwa wote katika kisanga hicho cha baa walikuwa 11 (miongoni mwao wanawake wawili) na ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika kituo cha polisi cha Maragua wakingoja kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Bw Keter alisema kuwa vita dhidi ya ukiukaji wa masharti ya kupambana na Covid-19 yataendelezwa na pia harakati za kutokomeza ujambazi wa kila aina ziambatane ili amani na uthabiti zinawili ndio wenyeji wajiingize katika ujenzi wa maisha yao na pia taifa lao bila utata wowote wa kuhangaishwa na wahalifu.

“Nawahakikishia wenyeji wa Maragua na viunga vyake na pia eneo letu lote kwamba tunajua ujambazi umekuwa na ujasiri wa kipekee hapa lakini sisi nasi tumejibu kwa ujasiri zaidi. Mmeshuhudia mwamko mpya katika harakati zetu eneo hili na ninawahakikishia kuwa hata hao ambao mnajua bado hatujawakamata, mipango ikon a hakuna hata mmoja atatulemea,” akasema.

[email protected]

You can share this post!

Mamia ya wasichana wafanyia KCSE hospitali baada ya...

Wazazi walia kanuni za corona zinaumiza watahiniwa wa KCSE