• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Maamuzi tofauti ya korti yaibua utata kesi ya polisi

Maamuzi tofauti ya korti yaibua utata kesi ya polisi

Na BRIAN WASUNA

MAAFISA wa polisi wanaopinga kufutwa kazi kwao miaka kadhaa iliyopita walipofeli zoezi la ukaguzi kuhusu maadili, wamegawa mahakama huku majaji wakitoa maamuzi yanayotofautiana katika kesi walizowasilisha kwa misingi iliyofanana.

Maamuzi hayo yamefanya baadhi ya maafisa hao kurudishwa kazini licha ya kushindwa kueleza Huduma ya Taifa ya Polisi (NPSC) walivyopata utajiri wao.NPSC ilipatiwa jukumu la kuwaondoa maafisa fisadi kutoka mojawapo ya idara zilizokolewa na uovu huo nchini.

Ukaguzi huo ulioongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa NPSC Johnston Kavuludi, ulianza Novemba 25, 2013 kulingana na katiba ambayo ilipitishwa mwaka wa 2010.Bw George Mburugu Ikiara alikuwa amepanda cheo hadi Inspekta Mkuu wa polisi alipopigwa msasa na tume hiyo mnamo Agosti 23, 2016.

Tume ilipata kwamba hakuweza kuthibitisha alivyopata pesa katika akaunti yake na kwamba alishirikiana na wakubwa wake wanne – Kennedy Obusuru Rucho, Polycarp Akoko Ochieng, Peter Katheka na John Wainaina Laban kwa kutumiana mamilioni ya pesa kupitia Mpesa.

Ikiara na wenzake walipoulizwa sababu ya kutumiana kiwango kikubwa cha pesa, walieleza kwamba walikuwa wakifanya biashara.Hata hivyo, kila moja wao alitaja biashara tofauti kama chanzo cha Sh3.3 milioni walizoshukiwa kupata kwa njia isiyo halali.

Bw Ikiara alisema alikuwa akiuza nguo, Ochieng akataja mahindi na huduma za mtandao, Rucho na wenzake wakataja biashara tofauti.Wote walifutwa kazi.

Lakini wiki jana, Jaji wa Mahakama Kuu James Rika alikubali malalamishi ya Bw Ikiara kwamba NPSC ilikosea kwa kupuuza kwamba alikuwa amehudumu kwa miaka 24 na alikuwa akipata mikopo kutoka chama cha akiba na mikopo.

Alipokuwa akitoa uamuzi wake, Jaji Nzioki wa Makau alikuwa akisoma uamuzi katika kesi ya Bw Ochieng aliyekuwa amewasilisha malalamishi sawa na ya Bw Ikiara.Jaji Makau aliamua kwamba NPSC ilifanya kazi yake na haikukosea kumfuta kazi Bw Ochieng .

Maamuzi hayo mawili yamefichua ugumu wa masuala ya kisheria wakati kesi mbili zinazofanana zinavyoamuliwa tofauti.Miaka mitano iliyopita, Jaji George Odunga, alimrudisha kazini afisa wa polisi Evans Momanyi Getembe akisema kwamba baadhi ya makamishna wa NPSC hawakuhudhuria vikao vya kumpiga msasa lakini walishiriki kupendekeza afutwe kazi.

Katika uamuzi mwingine mwaka wa 2018, Jaji Hellen Wasilwa aliamua kwamba tume ilikosea kumfuta kazi afisa wa polisi Peter Kemboi Chemos.

You can share this post!

KCSE: Magoha aamrisha polisi wapokonywe simu wasifanikishe...

Raia 100 wa kigeni wakamatwa kwa kuwa nchini bila kibali