• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
DHULUMA ZA KIMAPENZI: Serikali yaitia adabu Homeboyz Radio

DHULUMA ZA KIMAPENZI: Serikali yaitia adabu Homeboyz Radio

Na MARY WANGARI

MAMLAKA ya Mawasiliano ya Kenya (CAK) imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya kampuni inayomiliki kituo cha Homeboyz Radio kutokana na matamshi yaliyotolewa na watangazaji wake yaliyovutia hisia kali nchini.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa CAK, Mercy Wanjau alisema kampuni hiyo imetozwa Sh1 milioni kama faini, baada ya watangazaji wake kumkejeli mhasiriwa wa dhuluma za kingono Jumatano.

“Mnamo Machi 26, 2021, Mamlaka ilipokuwa ikifanya kazi yake kama kawaida ya ukaguzi, iligundua kuwa Homeboyz Radio ilikuwa imetoa matamshi ya kudhalilisha dhidi ya wanawake katika kipindi chake cha asubuhi, Machi 25, 2021.”

“Matamshi hayo yalikuwa kinyume na kanuni kuhusu Sheria za Vipindi inayohitaji watangazaji kupeperusha vipindi vinavyozingatia maadili ya kijamii na kifamilia wakati wa saa zenye wasikilizaji wengi,”alisema Bi Wanjau.

Kando na faini, CAK imeamrisha shirika hilo kusitisha kipindi hicho mara moja kwa muda wa miezi sita hadi kituo hicho kitakapothibitisha kutimiza matakwa yote ya kisheria na kanuni za Mamlaka hiyo.

Aidha, kituo hicho kimeagizwa kupeperusha ombi la msamaha kwa mhasiriwa katika saa ambazo watu wengi husikiza kwa siku tano kuanzia jana, pamoja na kuchapisha tangazo la kuomba msamaha katika magazeti mawili maarufu nchini.

Kuhusu wafanyakazi wake, Mamlaka hiyo iliagiza wapatiwe mafunzo na kuhamasishwa kuhusu masuala ya kijinsia ambapo mafunzo hayo yatahitajika kuidhinishwa na Tume ya Kitaifa kuhusu Usawa wa Kijinsia na nakala yake kutumwa kwa CAK.

Wametakiwa pia kuhudhuria masomo kuhusu Kanuni za Vipindi yatakayoendeshwa na Mamlaka hiyo.Kituo hicho kimeagizwa kuhakikisha watangazaji wake wameidhinishwa na Baraza linalosimamia Vyombo vya Habari Nchini (MCK) na kutuma ushahidi wa kufuata masharti hayo kwa CAK.

Isitoshe, Homeboyz Radio imeamrishwa kufanyia marekebisho sera yake ya uhariri ili iambatane na matakwa ya sheria kuhusu jinsia.

Mkurugenzi huyo aliwaonya watangazaji dhidi ya kutoa matamshi ya ubaguzi kuhusu jinsia akisistiza kuwa suala hilo halikuwa kuhusu jinsia na kwamba hatua sawa na hizo za kinidhamu bado zingechukuliwa endapo mhasiriwa angekuwa mwanamume.

“Mamlaka inatilia maanani kanuni ya kujumuisha jinsia na kuheshimu tofauti katika maumbile. Watangazaji wanahimizwa kuzingatia uwajibikaji wa kiwango cha juu wanapofanya kazi yao na kujiepusha na ubaguzi wa kijinsia, kupigia debe visa vya wanaume kuwatendea ukatili wanawake na kueneza kasumba potovu dhidi ya wanawake na wanaume.”

“Mamlaka itaendelea kufuatilia kwa makini vipindi vinavyopeperushwa na vituo vya habari ili kuhakikisha vinazingatia sheria za sekta ya ICT pamoja na Sheria kuhusu Habari na Mawasiliano Kenya. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Homeboyz Radio ni pamoja na kuwaachisha kazi watangazaji hao watatu kwa kukosa nidhamu kazini,” ilisema taarifa kutoka kwa CAK.

You can share this post!

Raia 100 wa kigeni wakamatwa kwa kuwa nchini bila kibali

CORONA: Viongozi wa Kiislamu wakosoa masharti ya Uhuru