CORONA: Viongozi wa Kiislamu wakosoa masharti ya Uhuru

Na WACHIRA MWANGI

VIONGOZI wa kidini katika Kaunti ya Mombasa wametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kujadiliana nao kabla ya kuchukua hatua za dharura kama kusitisha mikusanyiko ya waumini katika sehemu za ibada.

Viongozi hao waliozungumza katika hafla tofauti waliipongeza serikali kwa juhudi zake dhidi ya virusi hivyo hatari lakini wakasisitiza kuwa wanahitaji kushirikishwa katika masuala yanayoathiri sehemu za ibada.

“Tunafurahia Masharti ya Afisi ya Rais kuhusu kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. Hata hivyo, tunasikitika kuwa maamuzi hayo huwa yanalenga kila mara sehemu za ibada. Haya ni maeneo ya faraja, matumaini na kuunganishwa kiungu, ambapo watu wanaweza kujinyenyekeza, kumlilia na kumwomba Mungu.

“Huwa tunasahau na kuwaruhusu watu kwenda sokoni na maeneo mengine kujiburudisha, ilhali tunafunga makanisa, misikiti na maeneo mengineyo ya ibada wakati ambapo tunahitaji kwa dhati kwenda mbele ya Mungu kuomba msamaha wake na uponyaji dhidi ya janga hili,” alisema Katibu Mkuu wa Muungano wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Badru Khamis.

Akizungumza baada ya kuhudhuria mafunzo kuhusu maadili yaliyotolewa na mashehe Al Azhar Al Shariff kutoka Cairo Misri, katika Msikiti wa Masjid Shibu eneo la Mwembe Tayari, Mombasa, Sheikh Khamis alielezea wasiwasi wake kuhusu mwezi mtakatifu wa Ramadhan unaokaribia.

“Tunaelekea mwezi mtakatifu wa Ramadan na tutatarajiwa kushiriki maombi mara kadhaa, haya yatafanyika vipi?” aliulizaMnamo Machi 26, Rais Kenyatta alitangaza mikakati zaidi kuhusiana na hali inayozidi kuzorota ya janga la Covid-19.

Masharti hayo yalizingatia kaunti tano zilizotangazwa kama “maeneo yaliyoambukizwa ugonjwa” ” – ambayo ni kaunti za Nairobi, Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru.Rais aliamrisha kuwa mikutano yote ya watu na mikusanyiko katika sehemu za ibada katika kaunti hizo isitishwe hadi taarifa nyingine itakapotolewa.

Sheria kwamba sehemu za ibada zinaruhusiwa kutumia thuluthi moja ya nafasi waliyonayo, itadumishwa katika kaunti nyinginezo.

Habari zinazohusiana na hii