• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
Gavana Nyong’o aongoza Nyanza kumuomboleza Mama Sarah Obama

Gavana Nyong’o aongoza Nyanza kumuomboleza Mama Sarah Obama

SAMMY WAWERU na WANGU KANURI

GAVANA wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o ameongoza wakazi wa kaunti za eneo la Nyanza kumuomboleza nyanya wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Bw Barrack Obama, Mama Sarah Obama aliyefariki mapema Jumatatu.

Mama Sarah aliaga dunia katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi, Kisumu, saa kumi na dakika arubaini na tano alfajiri, ambapo alikuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi. Alilazwa humo Jumapili asubuhi.

“Tunatuma risala za pole kwa familia ya Obama na watu wa Kogelo, Kaunti ya Siaya kwa jumla. Wakenya tutamkosa sana,” inaeleza taarifa ya Prof Nyang’o kwa vyombo vya habari.

Akimtaja kama mama mchangamfu na mkarimu, gavana huyo amesifia mchango na utendakazi wake katika jamii, hasa kutokana na Wakfu wake wa Masomo wa Mama Sarah (Foundation), uliolenga kutoa ufadhili wa karo na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi kwa wanafunzi wasiojiweza.

“Ni kwa uchungu mwingi na majuto ningependa kutangaza kifo cha Mama Sarah Obama katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga katika kaunti ya Kisumu hii leo asubuhi baada ya ugonjwa mfupi. Mama Sarah alikuwa nyanya yake aliyekuwa Rais Barrack Obama wa Marekani. Wakenya watamkosa sana. Mama Sarah alikuwa mwenye moyo wa ukarimu haswa kwa wale waliomtembelea nyumbani kwake, Kogelo. Alikuwa rafiki yake marehemu mamangu na nyanya mwema kwetu sote. Mama Sarah hakuwa tu kielelezo kwa familia ya Obama lakini pia umbo la mama kwa watu wengi. Alikuwa mfadhili ambaye aliunganisha fedha na kulipa karo za watoto wengi mayatima na watoto walio kwenye mazingira magumu. Aliwasaidia wajane pia. Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi,” akachapisha gavana wa kaunti ya Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o.

Mradi huo ukiwa eneo la Kogelo, Kaunti ya Siaya, anakotoka, umekuwa wa manufaa makubwa kwa mayatima, wajane na familia zisizojiweza kwa kuwapa chakula, mavazi na kuwalipia karo.

“Mama Sarah Obama hakuifaa familia ya Obama pekee, ila alikuwa mama wa wengi. Alikuwa mfadhili aliyesaidia kuchangisha fedha kulipia karo mayatima na watoto wanaotoka familia zisizojiweza katika jamii. Vilevile, alisaidia wajane,” akafafanua Prof Nyong’o.

“Familia ya Obama ipo kwenye fikra na maombi yetu kwa kumpoteza Mama Sarah Obama. Alidhihirisha nguvu za kifamilia za kimitara za Kiafrika huku uwepo wake ukihisiwa mpaka ikulu ya rais ya Marekani,” akasema Dkt Boni Khalwale.

“Risala zangu za rambirambi zinaiendea familia ya Rais Barrack Obama kwa kuaga kwa Mama Sarah Obama. Atakumbukwa kwa mapenzi yake ya elimu na riadha lakini pia kwa juhudi zake katika kuinua na kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika mazingira magumu katika jamii. Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi,” akasema Bw Musalia Mudavadi.

Mama Sarah na ambaye alikuwa mjane na mke wa tatu wa babu ya Rais Obama, ametajwa kuwa ‘mwalimu’ na mfadhili aliyejali maslahi ya jamii.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 99, na kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia atazikwa baadaye leo, ikizingatiwa kuwa dini yake ni ya Kiislamu.

Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga pia ametuma salamu za pole. “Kwa kufariki kwake Mama Sarah Obama, tumempoteza mama aliyeishi kabla ya wakati wake. Kivyake, alihakikisha kuwa familia yake inaendelea hata baada ya mume wake kufariki,” akaandika Bw Raila Odinga.

Marehemu Sarah alizaliwa mnamo 1922 na ameaga akiwa na miaka 99 katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga katika kaunti ya Kisumu, Jumatatu. Mwendazake alifariki baada ya ugonjwa mfupi.

Mama Sarah kama alivyofahamika sana na watu, alimpokea Rais Obama wakati ambapo rais huyo alikuwa nchini Kenya. Katika safari yake, Rais Obama alikuwa amepania kuona kule babake aliishi eneo la Kogelo, magharibi mwa nchi Kenya.

Bi Sarah alikuwa mlezi wa Rais Obama akiwa mchanga. Hii ni baada ya mamake kuondoka akiwa mchanga. Itakumbukwa kuwa Bi Sarah ndiye alieleza kuwa mizizi ya Rais Obama ilikwenda mpaka nchini Kenya.

Marehemu Bi Sarah alianzia mradi wa Mama Sarah Obama ambapo huduma ya mradi huu iliegemea kuwasaidia mayatima, familia maskini na pia kuwaelimisha watoto wanaotoka katika familia hizo. Kupitia mradi huu Mama Sarah alinuia kuwasaidia watu sana hata ingawa hakupata elimu rasmi mwenyewe aliamini kuwa elimu ina manufaa mengi kwa watu.

 

 

You can share this post!

CORONA: Viongozi wa Kiislamu wakosoa masharti ya Uhuru

Watanzania mitandaoni wawafafanulia Wakenya maana ya neno...