• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Mama Sarah Obama kuzikwa Jumanne

Mama Sarah Obama kuzikwa Jumanne

Na SAMMY WAWERU

MAMA Sarah Obama, ambaye ni nyanya ya aliyekuwa Rais wa Amerika, Bw Barack Obama atazikwa kesho, Jumanne kwa mujibu wa itikadi za dini la Kiislamu.

Alifariki mapema Jumatatu, katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi, Kisumu, ambapo alikuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Aidha, familia yake imepuuzilia mbali tetesi zinazosambaa mitandaoni, zikidai aliaga kutokana na virusi vya corona. Imesema alifariki kutokana na maradhi ya kawaida.

Kulingana na Sheikh Musa Ismail, aliyezungumza kwa niaba ya familia, mwili wa Mama Sarah utasafirishwa hadi Kogelo, Kaunti ya Siaya anakotoka, na kuzikwa kesho kabla ya saa sita mchana.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake, Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ni kati ya viongozi wakuu serikalini na wanasiasa waliotuma salamu za pole kumuomboleza.

Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o akihutubia wanahabari katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi, alimtaja Mama Sarah kama mama aliyependa wageni.

“Sisi ambao tulipata fursa ya kuenda kwake mara nyingi, alikuwa mama aliyependa wageni. Isitoshe, alikuwa rafiki wa karibu na wa dhati wa mama yangu,” akasema Prof Nyong’o, akitoa salamu za pole kwa familia, jamaa, wakazi wa Kogelo anakotoka na eneo la Nyanza kwa jumla.

Gavana huyo alisema serikali ya kaunti ya Kisumu itashirikiana kwa karibu na ile ya Siaya katika maandalizi ya maziko ya Mama Sarah na aliyefariki akiwa na umri wa miaka 99.

“Kwa wakazi wa Kisumu, Kogelo – Siaya na Nyanza kwa jumla tumshukuru Mungu kwa kutupa Mama Sarah na mengi aliyotufanyia kimaendeleo. Tunazishukuru hospitali zilizomhudumia, zilijaribu kadri ya uwezo wao,” akaelezea Gavana Nyong’o.

Gavana wa Siaya, Bw Cornel Rasanga kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari pia alituma salamu za pole, akimuomboleza Mama Sarah kama “mama kiongozi mkarimu aliyejitolea kwa hali na mali kuiimarisha jamii”.

“Nimemjua Mama Sarah Obama kama mama mkarimu, aliyejawa na upendo, kujali na kusaidia wasiojiweza katika jamii,” Bw Rasanga akasema.

Mama Sarah alitumia Wakfu wake wa Mama Sarah Obama (Foundation) kuwalipia karo mayatima na watoto waliotoka katika familia maskini, zisizojiweza.

Pia atakumbukwa kutokana na jitihada zake kuinua mtoto wa kike nchini, kusaidia wajane, na kuwapa vyakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi wasiojiweza.

Alikuwa mke wa tatu wa babu ya Rais Barack Obama, na alitumia fursa ya kiongozi huyo akiwa madarakani Amerika kutafuta wafadhili na kufanya michango nchini humo.

You can share this post!

Watanzania mitandaoni wawafafanulia Wakenya maana ya neno...

Mama Sarah Obama alikuwa mwanamke wa kipekee – Raila...