• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Afueni kwa wakazi wa Machakos Gavana Mutua akiwapunguzia gharama ya maisha

Afueni kwa wakazi wa Machakos Gavana Mutua akiwapunguzia gharama ya maisha

Na SAMMY WAWERU

IMEKUWA afueni kwa wafanyabiashara na wakazi Machakos baada ya Gavana wa Kaunti hiyo Dkt Alfred Mutua kutangaza Jumatatu kuondoa na kupunguza kodi mbalimbali zinazohitajika kuendesha biashara.

Hatua hiyo hata hivyo ni ya muda ili kuwaondolea gharama ya juu ya maisha, kipindi hiki taifa na ulimwengu umezongwa na janga la Covid-19.

Kwenye barua iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Dkt Mutua ameorodhesha hatua na mikakati 10 inayolenga kuleta afueni kwa wafanyabiashara na wakazi katika kaunti hiyo.

Inajumuisha; Kuondoa malimbikizo ya riba na utozaji wa faini, adhabu kwa wamiliki wa ardhi kwa asilimia 100 kwa muda wa siku 45 zijazo, wahudumu wa matatu kupunguziwa kwa asilimia 50 ada ya kila mwezi wanayotozwa, kina mama mboga, wahudumu wa bodaboda, tuktuk na maruti kuondolewa kodi na malipo wanayotakiwa kulipa na halmashauri ya jiji katika maeneo yao ya kazi.

Katika afueni hiyo iliyoonekana kulenga wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri, Gavana Mutua pia ametangaza kusimamisha malipo ya ugawanyaji ardhi kwa muda wa miezi mitatu mfululizo na ada ya leseni za biashara ndogondogo kukabiliana na majanga ya moto mwaka huu wa 2021.

“Nimepunguza kwa asilimia 50 ada ya usafirishaji bidhaa Machakos, ikiwa ni pamoja na ada ya uegeshaji magari ya kuzisafirisha. Pia ninapunguza kwa asilimia 50 ada inayotozwa leseni za shule za kibinafsi na taasisi za elimu ya juu,” akaelezea Dkt Mutua.

Kwa ushirikiano na maduka ya kijumla ya Mulley kote nchini, serikali ya kaunti ya Machakos imetangaza kupunguza bei ya baadhi ya bidhaa za kula na za matumizi muhimu ya kimsingi ambazo ni pamoja na unga, mafuta ya kupikia, maziwa, mkate, sabuni na shashi (tissue paper).

“Ninashukuru kwa dhati maduka ya kijumla ya Mulley kwa ukarimu wenu kusimama na watu wetu kipindi hiki kigumu, kujinyima kupata faida na kukubali kugharamika kwa sababu mnajali maisha ya binadamu kuliko pesa. Mungu awabariki sana,” Dkt Mutua akaridhia hatua hiyo, akihimiza sekta zingine katika biashara kuiga mfano huo kuokoa Wakenya wanaohangaika kipindi hiki makali ya virusi vya corona yanazidi kuwalemea.

Ni hatua ambayo imeonekana kugusa nyoyo za wengi, wananchi wakielekeza shukrani zao mitandaoni.

“Hongera gavana, tukiwa na viongozi watatu kama wewe Kenya mwananchi wa kawaida atapata nafuu,” #Florence Chepkemoi akaridhia.

“Hii ni habari njema kuwapa afueni Wakenya katika kaunti yako wanaoumia kwa sababu ya corona. Umepiga hatua mbele kuliko viongozi wengine, wafuate nyayo zako,” akahimiza Steven Kamau.

Athari za corona hasa kutokana na sheria na mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia maenezi zaidi, zinaendelea kuyumbisha uchumi, gharama ya maisha ikipanda.

You can share this post!

Serikali yaonya wanaopandisha nauli kiholela

ODM WAONYA UHURU