• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
ODM WAONYA UHURU

ODM WAONYA UHURU

Na CHARLES WASONGA

BAADHI ya washirika wa kisiasa wa karibu wa kinara wa ODM Raila Odinga wamepuuzilia mbali madai kwamba kuna njama ya kuzima ushawishi wake nchini wakisema juhudi hizo zitaambulia patupu.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi pia waliwataja watu wanaoendeleza njama kama hiyo maadui wakubwa kwa juhudi za kuleta umoja nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Vile vile, wanasiasa hao walionya Rais Kenyatta wakisema hatua kama hiyo itavuruga utangamano uliotokana na handisheki kati yake na kiongozi huyo wa ODM.

Bw Wandayi, ambaye pia ni mkurugenzi wa masuala ya siasa katika ODM, alionya kuwa njama hiyo, ya kumtenga Odinga pia itavuruga mchakato wa BBI.“Watu wanaoendeleza njama hiyo chafu wajue kwamba wataleta migawanyiko nchini kwani juhudi zao zitahujumu handisheki na BBI. Kenya haiko tayari kuelekea mkondo huo,” akasema Mbunge huyo wa Ugunja.

“Tumesikia fununu kwamba maafisa wa fulani wakuu serikalini wanaendesha mipango kama hiyo. Lakini nawaambia kuwa hawatafaulu kwa sababu baba yuko mbioni kuunda muungano mpya wa kisiasa utakaokuwa na ushawishi kote nchini,” Bw Mbadi ambaye ni kiongozi wa wachache bungeni aliambia Taifa Leo.

Jana, iliripotiwa kuwa maafisa wenye ushawishi mkubwa serikalini wanaendesha mipango ya kudhoofisha ushawishi wa Odinga nchini kumfaidi mgombeaji fulani wa urais.

Njama hiyo inajumuisha kupigwa jeki kwa muungano wa “One Kenya Alliance” unaoshirikisha waliokuwa washirika wa Odinga katika muungano wa Nasa na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi. Wao ni kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.

Mbw Mudavadi na Wetang’ula wanatarajiwa kumfungia Bw Odinga katika ngome yao ya Magharibi mwa Kenya huku Bw Musyoka akizima nyota yake katika eneo la Ukambani.

Mkakati huo wa kumlemaza Bw Odinga kisiasa, pia unajumuisha juhudi za kuvuruga ushawishi wake katika ngome yake ya Pwani.

Juzi, Rais Uhuru Kenyatta alikutana na magavana watatu wa Pwani; Ali Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi) na Salim Mvurya (Kwale) ambapo inadaiwa walijadili “masuala ya maendeleo Pwani,”

Lakini duru zinasema kuwa suala la kuundwa kwa chama cha pwani kuzima ushawishi wa ODM lilijadiliwa kwa kina. Bw Odinga alipinga vikali wazo hilo katika ziara yake ya siku tano enoe la Pwani kuupigia debe mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Katika chaguzi za 2013 na 2017, Bw Odinga alipata kura nyingi zaidi katika maeneo ya magharibi, Ukambani na Pwani kufuatia uungwaji mkono wa vigogo wa kisiasa kutoka maeneo hayo.

Mapema mwezi huu, Seneta wa Siaya James Orengo alimlaumu Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho kwa kuendesha njama ya kuzima ndoto ya Bw Odinga kuingia Ikulu 2022.

“Tunawaonya maafisa kama hao kwamba hakungekuwa na handisheki kati ya Raila na Uhuru na ambao umezaa mchakato huu wa BBI, hawangepata nafasi ya kupanga urithi wa urais wanavyofanya,” akasema katika halfa moja ya mazishi katika eneo bunge la Rarieda, kaunti ya Siaya. Naye Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alidai, bila kutoa ithibati, kuwa Dkt Kibicho ndiye alichangia kushindwa kwa mgombeaji wao, David Were katika uchaguzi mdogo wa Matungu, kaunti ya Kakamega.

Bw Sifuna alidai, Katibu huyo alifadhili kampeni za mgombeaji wa ANC Oscar Nabulindo ili “kutoa taaswira kwamba umaarufu wa Raila katika magharibi mwa Kenya umedidimia kabisa,”

Hata hivyo, mnamo Alhamisi wiki jana, Bw Sifuna alidokeza kuwa ODM inapanga kuunda muungano wa kisiasa “utakaotikisa ulingo wa siasa nchini.”

“Rekodi yetu ya kuunda miungano, kujenga madaraja wanaochukuliwa kuwa maadui wetu na kuwakuza viongozi wenye nguvu inajulikana. Kwa mara nyingine tunapanga kufanya hivyo,”akasema huku akitaja muungano wa One Kenya Alliance kama wa kikabila.

You can share this post!

Afueni kwa wakazi wa Machakos Gavana Mutua akiwapunguzia...

Pigo kwa BBI corona ikiyumbisha refarenda