• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Pigo kwa BBI corona ikiyumbisha refarenda

Pigo kwa BBI corona ikiyumbisha refarenda

Na BENSON MATHEKA

TABIA ya wanasiasa ya kupuuza kanuni za kuzuia msambao wa virusi vya corona wakipigia debe mswada wa kubadilisha katiba, sasa imeweka mchakato huo kwenye hatari baada ya vikao vya bunge kusitishwa ikiendelea kushughulikia mswada huo.

Ingawa wabunge wanakutana kesho kujadili mswada wa kusitisha vikao kufuatia tangazo la Rais, wadadisi wanasema kwamba hatua hiyo itayumbisha mipango ya vinara wa mchakato huo wa kufanyika kwa kura ya maamuzi Juni mwaka huu.

Maspika wa bunge la kitaifa na seneti walikuwa wameashiria kwamba mswada huo ungeshughulikiwa haraka ili muda uliowekwa wa kukamilisha mchakato huo uafikiwe.

Vinara wa mchakato huo wamekuwa wakisema kwamba kura ya maamuzi itafanyika Juni mwaka huu na kisha utekelezaji wa mageuzi mengine ya kiusimamizi kukamilishwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Kufikia Ijumaa iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza hatua kali za kukabili wimbi la tatu la corona ikiwemo kusimamishwa kwa vikao vya bunge, kamati za sheria na Seneti zilikuwa zikijadili jinsi ya kuushughulikia.

Miongoni mwa hatua ambazo Rais Kenyatta alitangaza ni bunge kusitisha vikao vikiwemo vya kamati kwa muda usiojulikana hatua ambayo baadhi ya wadadisi wanasema inaweza kuathiri kura ya maamuzi.

“Kwa makubaliano na uongozi wa mabunge yote mawili na uongozi wa kaunti, vikao vya bunge vikiwemo vya kamati mbali mbali za mabunge ya Kaunti za Nairobi, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nakuru, vimesimamishwa hadi itapotangazwa tena,” Rais alisema.

Spika wa Bunge Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka walikuwa Ikulu Rais alipotangaza kusitishwa kwa vika vya bunge ikiwa ni pamoja na kufunga kaunti za Nairobi, Machakos, Kajiado, Nakuru na Kiambu.

Mbali na kusitisha vikao vya bunge, Rais Kenyatta, pia alidumisha marufuku ya mikutano ya kisiasa, ambayo ililaumiwa kwa kuchangia wimbi la tatu la corona.

Hii ni pigo kwa wabunge ambao walipanga kuandaa vikao vya kupokea maoni kutoka kwa umma kuhusu mswada huo.

Baadhi ya viongozi waliokuwa msitari wa mbele kupuuza kanuni za wizara ya afya kwa kuandaa mikutano ya hadhara kupigia debe mswada huo akiwemo kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wameambukizwa virusi hivyo.

Wabunge na maseneta kadhaa ambao wanafaa kujadili mswada huo kabla ya kuwasilishwa kwa Rais pia wameambukizwa virusi hiyo na kujitenga wapone.

Mnamo Jumamosi, Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo na Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata walitangaza kuwa wameambukizwa corona na wamejitenga kulingana na kanuni za wizara ya afya.

Joto la kisiasa ambalo lilikuwa limepanda wanasiasa wakitoa hisia zao tofauti kuhusu mswada huo lilitulia serikali ilipotangaza kuwa Kenya inakumbwa na wimbi la tatu la maambukizi ya corona.

Naibu Rais William Ruto na washirika wake ambao walikuwa wakiandaa mikutano kupinga kura ya maamuzi kupitia kampeni ya hasla pia wametuliza boli.

Duru zinasema baadhi yao wameambukizwa virusi vya corona.

You can share this post!

ODM WAONYA UHURU

Rais Suluhu aanza kazi kwa kutumbua majipu