• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Rais Suluhu aanza kazi kwa kutumbua majipu

Rais Suluhu aanza kazi kwa kutumbua majipu

Na THE CITIZEN

SIKU chache tu baada ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu ameanza kuchapa kazi kwa kumtimua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) Dusdedit Kakoko aliyetajwa kwenye ripoti ya ufisadi iliyotolewa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Jumamosi.

Rais Suluhu alichukua usukani kufuatia kifo cha mtangulizi wake marehemu John Pombe Magufuli aliyezikwa mnamo Ijumaa wiki jana na tayari ameanza kuwakabili watu wanaotuhumiwa kuwa wafisadi katika idara mbalimbali za serikali.

Rais Suluhu alimfuta kazi mkurugenzi huyo baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo katika ikulu ya Dodoma, akisema kuwa kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha katika mamlaka hiyo. Pia aliitaka Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini humo (PCCB) iwachukulie hatua waliohusika na ufisadi huo.

Aidha alisema kuwa alifahamu kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa amebuni jopo kuchunguza matumizi mabaya ya fedha yaliyokuwa yakiendelea katika bandari hiyo kisha hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

“Kutokana na ripoti ambayo iliwasilishwa kwangu Jumamosi, zaidi ya Sh3.6 bilioni zilizopotea katika TPA. Wakati ambapo Waziri Mkuu aliagiza uchunguzi ufanyike, wafanyakazi wa chini ndio walifutwa huku wale wa ngazi ya juu wakiachwa nje. Sasa naamrisha mkurugenzi mkuu asimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi kuhusu ufisadi huu,” akasema.

Mnamo Disemba mwaka jana, Majaliwa aliwasimamisha kazi maafisa wawili wa TPA ambao ni wa ngazi ya chini ili kupisha uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. Wawili hao waliotimuliwa ni mkurugenzi wa kitengo cha fedha Nuru Mhando na mwenzake anayeidhinisha matumizi ya pesa Witnes Mahela.

Wakati huo Majaliwa alisema kuwa kuondolewa kwa ushuru wa Sh2 bilioni kwa kampuni ya saruji ya Mbeya haikufaa kwa kuwa hatua hiyo ilikataliwa na kamati maalum iliyoundwa kuamua kuhusu suala hilo.

Rais Suluhu pia alisema jana kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wakurugenzi wengine wa kampuni mbalimbali waliotajwa kwenye ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali aliyokabidhiwa, akisema serikali yake haitavumilia wafisadi.

Kakoko aliyetimuliwa, alipokezwa wadhifa wa mkurugenzi wa TPA mnamo Oktoba 2018 baada ya kushikilia wadhifa huo kama kaimu mkurugenzi kwa muda mrefu.

Aliuchukua kutoka kwa Awadhi Massawe ambaye pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu kwenye wizara hiyo Shaaban Mwinjaka, walifutwa kazi na Rais Magufuli baada ya kupotea kwa makontena 2,700 ya mizigo bandarini.

You can share this post!

Pigo kwa BBI corona ikiyumbisha refarenda

Mwanamke mwenye ndevu asimulia jinsi alivyojikubali