Mshtuko huku corona ikiua maafisa 5 wa kaunti

Na COLLINS OMULO

WIMBI la tatu la ugonjwa wa Corona limeathiri pakubwa kaunti ya Nairobi ambapo wafanyakazi watano walipoteza maisha yao mnamo Jumamosi pekee kutokana na ugonjwa huo.

Wafanyakazi hao wamekuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali kote nchini baada ya kuambukizwa virusi hivyo hatari.

Maafisa hao ni pamoja na mhudumu katika afisi ya uendeshaji mashtaka chini ya idara ya sheria, mwelekezi wa chumba cha mazoezi katika City Stadium, mfanyakazi mwanamume katika Afisi ya kutoza Kodi, mfanyakazi mwanamke katika Idara ya Kupima Thamani na dereva mmoja.

Vifo vya maafisa hao vilimchochea naibu gavana Anne Kananu kutoa tangazo Jumapili kuchukua hatua za dharura kwa kufunga afisi zote zisizotoa huduma muhimu kwa siku 30, ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.

“Hii ni hatua iliyotathminiwa kwa makini ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa maambukizi hatari ya Covid-19 yaliyoshuhudiwa katika siku za hivi majuzi,” alisema Bi Kananu.

Alieleza kwamba, mkurupuko mpya wa janga la Covid-19 umekuwa ukienea kwa kasi na umesababisha vifo vya maafisa wa kaunti, familia na marafiki.

Amri hiyo ya kufunga shughuli iliyoanza jana, ilibakisha tu afisi zinazotoa hudumu muhimu na za dharura zitakazoendelea pasipo kukatizwa.

Idara hizo zinajumuisha huduma za afya, usimamizi na udhibiti wa majanga (maafisa wa zima moto) huduma za kukusanya mapato, maji, mazingira na usafi, mipangilio ya fedha na uchumi, huduma za ununuzi na usambazaji, huduma za ulinzi, mawasiliano ya umma na huduma kwa wateja.

Habari zinazohusiana na hii