• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Kilio Kaunti ya Mombasa kuamuru wakazi watumie daraja jipya badala ya feri

Kilio Kaunti ya Mombasa kuamuru wakazi watumie daraja jipya badala ya feri

Na WINNIE ATIENO

Vurugu zinatarajiwa leo katika kivukio cha Likoni baada ya kamati ya dharura ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kaunti ya Mombasa kuagiza zaidi ya abiria 300,000 kutumia daraja la Likoni badala ya feri.

Zaidi ya abiria laki 300,000 hutumia kivukio cha Likoni kuvuka kutoka kisiwani Mombasa hadi Pwani Kusini. Hata hivyo msongamano katika feri sita zinazovusha abiria kutoka pande zote mbili imesababisha kamati hiyo kutafuta suluhu ili kuepuka janga la corona.

Kivukio cha feri kilitajwa kama mojawpao ya sehemu hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Daraja hilo lililojengwa mwaka jana kwa gharama ya Sh1.9 billion ilinuia kukabiliana na msongamano wa abiria wanaovuka kutumia feri.

Hata hivyo licha ya kuwepo kwa daraja hilo wakazi wengi wangali wanatumia feri kuvuka wakitaja changamoto kadha wa kadha ikiwemo jua kali, umbali na ukosefu wa magari ya umma kuwasafirisha hadi Liwatoni ambako daraja hilo ilipo hadi mjini Mombasa.

Kamati hiyo inayoongozwa na kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo na Gavana Hassan Joho imekuwa ikishurutisha wakazi kutumia daraja hilo bila mafanikio.

“Kwanzia leo, matatu zitakuwa zikisafirisha abiria hadi Liwatoni ili watu waanze kutumia daraja la Likoni kupunguza msongamano kwenye feri,” alisema naibu kamishna wa kaunti ya Mombasa Martin Mbae.

Jumatano, kamati hiyo ikiongozwa na vyombo mbalimbali za serikali ikiwemo halshamauri ya barabara kuu nchini, Huduma za Feri nchini, Mamlaka ya Bandari nchini, viongozi wa kidini na serikali ya kaunti ya Mombasa waliweka mapendekezo ya kukabiliana na janga hilo kwenye mkutano wa dharura.

Bw Mbae alisema sheria hizo zitaongoza kamati hiyo kupambana na janga hilo.

Kwenye mapendekezo hayo, wageni wote wanaozuru Mombasa watatakiwa kuwasilisha barua maalum ya kuonyesha hawana virusi vya corona katika mipaka ya mji huo wa kitalii.

Kaunti hiyo imesema imezindua shughuli ya kuwapa watu chanjo dhidi ya Corona kwenye mipaka ya kuingia na kutoka Mombasa.

Vile vile, kamati hiyo ya kukabili janga la corona iliagiza kufungwa mara moja kwa muda usiojulikana shule zote zinazowafunza watoto dini ambazo ni madrassa na Sunday School.

Kamati hiyo ilisema hatua hiyo ni ya kuwaepushia watoto kuendelea kuwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Corona.

Watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi wamekatazwa kuhudhuria ibada makanisani na misikitini na makongamano yenye watu wengi.

“Wazee hawafai kuhudhuria mikusanyiko ya kidini sababu tumegundua kuwa asilimia 90 ya vifo miongoni mwa kundi hilo inatokana na virusi hivyo,” alisema Bw Mbae.

You can share this post!

Hatimaye Ruto apokea chanjo ya corona

KCSE: Afisa abambwa na Magoha akisaidia watahiniwa kwa...