• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Ninafurahia BBI imesambaratika, tuliomba Mungu sana – Reuben Kigame

Ninafurahia BBI imesambaratika, tuliomba Mungu sana – Reuben Kigame

Na MWANGI MUIRURI

Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za kumtukuza Mungu, Bw Reuben Kigame sasa amejitokeza kusherehekea utata unaokumba mpango wa Maridhiano ya Kitaifa (BBI) akisema kuwa hali hiyo ni matendo ya Mungu.

“Tuliomba Mungu BBI isambaratike na kwa sasa hali imetuangazia kama waliokuwa kwa msimamo wa haki,” akasema.

Bw Kigame ambaye huwa na ulemavu wa kuona alikuwa akirejelea msimamo wa Muungano wa Maaskofu wa Kujitegemea nchini ambao wamekuwa wakiungana na baadhi ya makanisa mengine kudunisha mchakato huo wa BBI.

Alisema kuwa BBI kwa muda huu wote ni mradi ambao haukuwafaa Wakenya kwa lolote ikizingatiwa kuwa kuna changamoto nyingi ambazo zinafaa kupewa kipau mbele hasa katika safu ya kuwalegezea raia uhasi wa umasikini.

Bw Kigame alidai kuwa kuvurugika kwa mchakato huo kwa sasa ni matendo ya Maulana ambaye anataka kuwashinikiza viongozi wawe wa kufuatilia ya umuhimu kuhusu maisha ya wananchi.

Bw Kigame akitoa mfano wake wa mahangaiko alisema kuwa katika utekelezaji kipawa chake cha utunzi na uimbaji ameishia kubakia wa kunyonywa na matapeli katika sekta.

“Huku tukiwa na viongozi ambao kila kuchao wanadai vile wanatupenda na jinsi wanavyotuthamini. Wangekuwa wakweli wangenusaudia sambamba na wengine kuvuka haki ya vipawa vyetu,” akasema.

Alisema kuwa hukabidhiwa Sh18,000 kama marupurupu ya utumizi wa usanii wake, akitaja pato hilo la kila mwaka kama utapeli.

 

‘Wanasiasa wasije kwa mazishi yangu’

Kutokana na unafiki wa viongozi, alisema kuwa akiaga dunia hangependelea kukumbukwa na wanasiasa kwa mazishi yake wala kuombolezwa nao. “Afisa yeyote wa serikali au Bodi ya Hakimiliki asiruhusiwe kuhutubu katika mazishi yangu.”

Alisema uongozi wa kweli unafaa kuwatilia maanani wanyonge katika Jamii na haki iwe nguzo muhimu ya kustawisha maisha ya wananchi. Bw Kigame aliongeza kuwa inafaa BBI igonge ukuta na isahaulike na Wakenya.

Alishambikia kuvurugika kwa hali sasa ambapo Mahakama imeweka referenda breki, bunge la kitaifa limezua makataa kuihusu huku hata mwasisi wayo–Kinara wa ODM Bw Raila Odinga kupitia wandani wake–wakijitokeza kusema hata referenda sio ya dharura.

Mwandani sugu wa Bw Odinga ambaye ni Gavana wa Kakamega Bw Wycliffe Oparanya amesema kuwa referenda katika mazingara ya Janga la Covid-19 na mikopo kiholela sio wazo la busara.

Amesema kuwa Wakenya hawafai kupiga kura ya referenda kabla ya Julai kama ilivyoratibiwa na mwezi wa nane mwaka ujao warejee kwa debe kushiriki Uchaguzi mkuu.

Utata huo ukiambatana na upinzani wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto na wakereketwa wa Linda Katiba ambao wanaongozwa na Kinara wa Narc Kenya Bi Martha Wangari Karua ndio Bw Kigame anautaja kuwa sawa na baraka–Matendo ya Mungu na dhihirisho kuwa, akidai, maombi hufanya Kazi.

Hata hivyo, kunao wamezindua njama ya kumkejeli wakimwambia ikiwa maombi huwa na nguvu hivyo, basi pia aombee Janga la Covid-19 nalo liwaondoke Wakenya na pia umasikini.

Lakini Bw Kigame amejibu kuwa hata Yesu Kristo katika imani alisulubiwa na kando yake msalabani akawa na pamoja na wezi wawili ambapo mmoja alikiri kuwa imani kwa Mungu huponya hata dhambi.

“Aliyekaidi hakuingia katika Ufalme wa Mungu…la mno likiwa hili ni somo mwafaka kwa Serikali ikome kusukuma mambo ambayo hayasaidii maisha ya Wakenya kuboreka,” akasema akiongeza kuwa binafsi hatachoka kuwaombea wenzake nchini kupungukiwa na shida.

You can share this post!

Shaffie Weru sasa afukuza Sh21 milioni akidai alipigwa...

Kampuni za dawa zaonya wananchi dhidi ya chanjo feki ya...