• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Lewandowski kukaa nje kwa mwezi mmoja baada ya kupata jeraha baya la goti

Lewandowski kukaa nje kwa mwezi mmoja baada ya kupata jeraha baya la goti

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Robert Lewandowski atasalia mkekani kwa mwezi mmoja ujao kuuguza jeraha la goti, jambo ambalo litamkosesha fursa ya kuchezea Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG).

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 aliondoka uwanjani akichechemea baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Poland dhidi ya Andorra katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2022 mnamo Machi 28, 2021.

Lewandowski alikuwa tayari ameondolewa katika orodha ya kikosi kilichokuwa kitegemewe na Poland katika mchuano mwingine wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Uingereza mnamo Machi 31, 2021 uwanjani Wembley.

“Alipata jeraha baya la misuli kwenye goti la kulia,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Bayern ambao ni miamba wa soka nchini Ujerumani.

Lewandowski kwa sasa yuko Ujerumani anakotibiwa na madaktari wa Bayern.

Bayern ambao kwa sasa wanaongoza msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), wameratibiwa kupepetana na RB Leipzig ligini mnamo Aprili 3, 2021.

Siku nne baadaye, mabingwa hao watetezi wa taji la Bundesliga watakuwa wenyeji wa PSG kwa ajili ya mkondo wa kwanza wa kipute cha UEFA kabla ya kurudiana na miamba hao wa soka ya Ufaransa jijini Paris mnamo Aprili 13, 2021.

Iwapo Bayern watafaulu kubandua PSG, basi huenda wakakosa pia maarifa ya Lewandowski kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali.

Mshindi wa michuano ya mikondo miwili ya robo-fainali kati ya Bayern na PSG atakutana ama na Manchester City au Borussia Dortmund kwenye mikondo miwili ya nusu-fainali itakayopigwa mnamo Aprili 27-28 na Mei 4-5, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo na Jota watambisha Ureno dhidi ya Luxembourg

Kocha Molefi Ntseki wa Bafana Bafana ya Afrika Kusini...