• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Cape Verde, Guinea-Bissau, Mauritania na Ethiopia pia wafuzu fainali za AFCON 2022

Cape Verde, Guinea-Bissau, Mauritania na Ethiopia pia wafuzu fainali za AFCON 2022

Na MASHIRIKA

MATAIFA ya Cape Verde, Guinea-Bissau, Mauritania na Ethiopia ndiyo yalikuwa ya mwisho kabisa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazoandaliwa nchini Cameroon mnamo 2022.

Cape Verde walishuka uwanjani mnamo Machi 30 wakihitaji sare ya aina yoyote dhidi ya Msumbiji ili kufuzu. Hata hivyo, walisajili ushindi wa 1-0 baada ya Faisa Bangai wa Msumbiji kujifunga.

Katika mchuano mwingine wa Kundi F, wenyeji Cameroon walilazimishiwa sare tasa na Rwanda.

Guinea-Bissau walifuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kupepeta Congo 3-0 katika uwanja wa Bissau 24 September.

Piqueti alifungulia Guinea-Bissau ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Alexandre Mendy na Jorginho kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao ambao wangefuzu iwapo wangesajili ushindi katika mechi hiyo ya Kundi I.

Katika Kundi E, Mauritania walisonga mbele baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) katika mchuano huo wa Kundi E uliosakatiwa jijini Banjul. Ushindi huo uliwapa tiketi ya kufuzu kwa pamoja na Morocco waliokuwa wenyeji wa Burundi.

Sare tasa iliyosajiliwa na Bukini (Madagascar) dhidi ya Niger ilimaanisha kwamba Ethiopia walifuzu kutoka Kundi K licha ya kuwa walikuwa wamepokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Ivory Coast kufikia dakika ya 80 ambapo mechi ilisimamishwa baada ya refa Charles Bulu kuanguka uwanjani.

Bulu alipelekewa hospitalini haraka baada ya kupokezwa matibabu ya huduma ya kwanza uwanjani.

Refa huyo alikuwa amejaza pengo la mwamuzi mwingine ambaye hakufika uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo. Refa ambaye angejaza nafasi ya Bulu naye alikuwa raia wa Ivory Coast, hivyo ikalazimu mchuano kusitishwa kuepuka suala la mgongano wa maslahi.

Kushindwa kwa Madagascar kupiga Niger waliovuta mkia wa Kundi K, kulimaanisha kwamba Ethiopia walifuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2013.

Kwingineko, mabao kutoka kwa Victor Osimhen, Oghenekaro Etebo na Paul Onuachu yalisaidia Nigeria kupepeta Lesotho 3-0 katika Kundi L. Katika mechi nyingine ya Kundi I, Senegal walifunga katika dakika za mwisho na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Eswatini (Swaziland).

Bado kuna nafasi moja zaidi ya kufuzu ili kujaza jumla ya vikosi 24 vitakavyonogesha fainali zijazo za AFCON 2022. Hii ni baada ya Benin kususia mechi yao ya Kundi L dhidi ya Sierra Leone jijini Freetown baada ya maafisa wa Sierra Leone kushikilia kwamba vipimo vya corona vilibainisha kuwa wanasoka watano wa Benin walikuwa na virusi vya homa hiyo hatari.

Ili kuungana na Nigeria walioongoza Kundi L, Sierra Leone walihitaji ushindi nao Benin walihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu kwa fainali za AFCON 2022. Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limesema mechi itasakatwa upya katika tarehe itakayotolewa baadaye.

TIMU AMBAZO ZIMEFUZU AFCON 2022:

KUNDI A: Mali, Guinea

KUNDI B: Burkina Faso, Malawi

KUNDI C: Ghana, Sudan

KUNDI D: Gambia, Gabon

KUNDI E: Morocco, Mauritania

KUNDI F: Cameroon, Cape Verde

KUNDI G: Misri, Comoros

KUNDI H: Algeria, Zimbabwe

KUNDI I: Senegal, Guinea-Bissau

KUNDI J: Tunisia, Equatorial Guinea

KUNDI K: Ivory Coast, Ethiopia

KUNDI L: Nigeria, Sierra Leone au Benin

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kocha Molefi Ntseki wa Bafana Bafana ya Afrika Kusini...

Serikali yazima matumaini ya michezo kurejelewa