• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Daraja la Liwatoni lazidisha hatari ya kuenea kwa corona

Daraja la Liwatoni lazidisha hatari ya kuenea kwa corona

Na WINNIE ATIENO

MPANGO uliotajwa kuwa wa kuzuia maambukizi ya Covid-19 jijini Mombasa umegeuka kuwa tisho kubwa zaidi la kueneza janga hilo.

Hii ni baada ya msongamano mkubwa wa watu kushuhudiwa jana katika Daraja la Liwatoni, baada ya zaidi ya watu laki tatu kulazimishwa kulitumia badala ya kuabiri feri.

Agizo hilo lilitolewa na kamati ya dharura ya kudhibiti Covid-19 katika Kaunti ya Mombasa, ikiwataka watu wanaotembea kutumia daraja hilo badala ya feri ili ‘kuepuka janga la corona.’

Lakini msongamano ambao kamati hiyo ilisema ilikuwa inataka kupunguza uliongezeka katika daraja hilo, na hivyo kuweka maisha ya wakazi katika hatari kubwa zaidi.

Daraja hilo linaloelewa baharini, lilijengwa mwaka jana ili kupunguza msongamano Likoni.Zaidi ya abiria laki tatu hutumia Kivuko cha Likoni kutoka Kisiwani Mombasa hadi Pwani Kusini kila siku. Akina mama wajazito na walemavu jana walielezea masaibu yao baada ya kushurutishwa kutumia daraja hilo badala ya feri.

“Tumeteseka sana wakati wa kuvuka kutokana na msongamano wa watu,” alisema Fatuma Pingu mkazi wa Likoni.Naye Bi Aisha Mohammed aliisihi serikali kuruhusu walemavu, wajawazito na wafanyibiashara kutumia feri badala ya daraja hilo wanaposafirisha vyakula kutoka soko la Kongowea.

Hata hivyo, Bw Chrispine Otieno, mkazi wa Likoni aliisifu serikali kwa hatua hiyo akisema itawalinda dhidi ya virusi vya corona.

“Feri zilikuwa na misongamano sana. Hii ni afueni kwetu, lakini polisi washike doria kuhakikisha kila mtu anavaa barakoa,” alisema Bw Otieno.

Daraja hilo litakuwa likifunguliwa kwa umma kuanzia saa kumi na moja alfajiri kabla ya kufungwa kuruhusu meli kupita, kisha kufunguliwa tena saa kumi hadi saa kumi na mbili jioni.

Kamati ya dharura inayoongozwa na kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Gilbert Kitiyo na Gavana Hassan Joho, imekuwa ikiwataka wakazi kutumia daraja hilo bila mafanikio tangu mwaka jana.

You can share this post!

BBI YAINGIA ICU

Wakazi wa Pwani kuhamishiwa bara