• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 8:55 AM
Hatimaye serikali yaungama chanjo ya AstraZeneca ina madhara

Hatimaye serikali yaungama chanjo ya AstraZeneca ina madhara

Na CHARLES WASONGA

KENYA imeungana na mataifa mengine ulimwenguni ambayo yameripoti athari za chanjo aina ya AstraZeneca inayolenga kuzuia maambukizi wa virusi vya corona.

Hii ni baada ya Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman Alhamisi kufichua kuwa Bodi ya Dawa na Sumu Nchini (KPPB) wakati huu inachunguza visa saba vilivyoripotiwa vya watu waliopata chanjo kupata madhara mabaya.

Alisema visa hivyo saba ni miongoni mwa jumla ya visa 263 vilivyoripotiwa kutoka sehemu mbali nchini.

Hata hivyo, Dkt Aman hakutoa maelezo zaidi kuhusu visa hivyo vya madhara ya AstraZeneca vinavyochunguzwa akiahidi kufanya hivyo baadaye juma lijalo.

“Ni kweli kwamba bodi ya dawa nchini inachunguzwa visa saba miongoni mwa visa 263 kuhusu madhara ya chanjo ya AstraZeneca vilivyoripotiwa. Wizara ya Afya kwa ushirikiano na bodi hiyo zitatoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo wiki ijayo. Hata hivyo, hamna sababu ya Wakenya kuingiwa na hofu kwa sababu nyingi za madhara hizo ni ya kawaida kama kupanda kwa joto mwili na maumivu ya mwili,” akawaambia wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Jumba la Afya, Nairobi.

Mataifa kadhaa katika bara Uropa yamesitisha shughuli ya utoaji chanjo ya AstraZeneca baada ya visa kadha vya watu kuganda damu, na hata kufariki, kugunduliwa.

Kufikia Alhamisi jumla ya watu 196,435 nchini walikuwa wamepokea chanjo hiyo wengi wakiwa wahudumu wa afya, maafisa wa usalama na walimu.

Baadaye kwenye kikao na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa Kenya inashirikiana na washirika wengine duniani kuhakikisha kuwa imepokea chanjo zaidi kuweza kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Kulingana na makadirio ya Wizara ya Afya, kufikia Juni, mwaka ujao serikali inakisia kuwa jumla ya Wakenya 26 milioni watakuwa wamepokea chanjo dhidi ya corona.

You can share this post!

Wanabiashara wapigia debe chama cha Pwani

Mreno aliyetuma droni kwa makazi ya Ruto ashtakiwa