• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Askofu ataka serikali ichanje Wakenya wote

Askofu ataka serikali ichanje Wakenya wote

Na TITUS OMINDE

ASKOFU wa Kanisa Katoliki anayesimamia dayosisi ya Eldoret, Dominic Kimengich, ameitaka serikali kutafuta dozi zaidi za chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona.

Akiwahutubia waandishi wa habari mjini Eldoret baada ya kuongoza ibada ya Pasaka, Askofu Kimengich alihimiza serikali ishughulikie changamoto ya ukosefu wa chanjo hiyo haraka.

Askofu Kimengich alisema kuna haja ya serikali kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kwamba Wakenya wote wamepewa chanjo dhidi ya virusi hivyo.

‘Ninasihi serikali ihakikishe kuna chanjo ya kutosha kukidhi matarajio ya Wakenya wengi ambao wanasubiri kupewa chanjo. Wakenya wote bila kujali matabaka yao katika jamii wana haki ya kupata kinga hiyo,” akasema Askofu Kimengich.

Askofu huyo alielezea matumaini yake kwa serikali kutafuta chanjo zaidi kupatiwa Wakenya ambao wako tayari kuchanjwa.Awali, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alisema serikali imepanga kuchanja Wakenya milioni 1.25 kati ya Februari na Juni, wakiwalenga zaidi wafanyikazi wa huduma za afya, polisi na walimu.

Awamu ya pili kulingana na Bw Kagwe inatarajiwa kuanza Julai 2021 hadi Juni 2022, wakati ambapo Wakenya milioni 9.7 zaidi watapokea chanjo hiyo.

Askofu Kimengich alimsifu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuzifunga kaunti tano katika vita dhidi ya virusi hivyo.Kasisi huyo alitoa wito kwa Wakenya kuzingatia hatua zote zilizowekwa na serikali katika vita dhidi ya msambao wa virusi vya corona.

Alisema idadi ya Wakenya walioambukizwa virusi hivyo imeendelea kuongezeka, na hivyo uamuzi wa Rais Kenyatta wa kuzifunga kaunti hizo tano unafaa.

‘Covid-19 inaendelea kuihujumu nchi yetu, kwa sasa kuna Wakenya wengi ambao wameambukizwa virusi hivi. Ulikuwa uamuzi wa busara kwa rais kuzifunga kaunti zilizoathiriwa kufuatia ushauri kutoka kwa wataalam,”alisema Askofu Kimengich.

Aliwataka Wakenya kutii maagizo ambayo yamekusudiwa faida ya nchi.

You can share this post!

Abdul Haji afuata nyayo za waliorithi jamaa zao kisiasa

Hakuna kulipa zaidi kuegesha magari jijini