One Kenya Alliance ina mchongoma wa kupanda kisiasa

Na WANDERI KAMAU

WAANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta wanakabiliwa na kibarua kigumu kuujenga muungano wa One Kenya Alliance, kwa kuvuruga uungwaji mkono wa Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika ngome zao.

Juhudi hizo ziliibuka wiki iliyopita, ilipobainika kwamba kumekuwa na njama fiche ambazo zimekuwa zikiendeshwa na maafisa wakuu katika Ikulu kufadhili shughuli za muungano huo.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Chama cha ODM kimekuwa kikilalamikia “kupendelewa” kwa muungano huo na serikali, hasa baada yake kuibuka mshindi kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu, Kabuchai na Kaunti ya Machakos.

Kufichuka kwa njama hizo ndiko kunakotajwa kuchangia Rais Kenyatta kumwendea kwa haraka Bw Odinga mnamo Jumatano, ili kuzima wasiwasi ambao ulikuwa umeibuka kuhusu handisheki na mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta alifanya kikao cha faragha na Bw Odinga katika makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi, ili kujaribu kumhakikishia kuwa kila kitu ki shwari.

“Rais Kenyatta alimhakikishia Bw Odinga kuwa kila kitu ki shwari,” zikaeleza duru.Licha ya mkutano huo, imeibuka kwamba huenda ikawa kibarua kigumu kwa wandani wa Rais Kenyatta kuujenga muungano huo, hasa ikiwa lengo lao ni kuvuruga ufuasi wa Dkt Ruto na Bw Odinga katika ngome zao.

Wadadisi wa siasa wanasema licha ya muungano huo kupata ushindi kwenye chaguzi ndogo kadhaa zilizopita, Dkt Ruto na Bw Odinga bado ni wanasiasa wenye ushawishi na ufuasi mkubwa sana katika ngome zao.

Vile vile, wanaeleza kwamba huenda njama hizo zikaimarisha uungwaji mkono wao miongoni mwa wafuasi wao, ikiwa itabainika kuwa lengo la muungano huo ni kuwaingilia kisiasa.

“Dkt Ruto na Bw Odinga ni viongozi ambao wana wafuasi wanaowaamini na kuwategemea sana. Ni wanasiasa wenye uwezo wa kuwaagiza wafuasi wao kufuata mwelekeo wowote wa kisiasa. Hivyo basi, ikiwa itabainika kwamba lengo la muungano wa One Kenya Alliance ni kuwaingilia, basi hilo huenda likawajenga hata zaidi,” akasema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kwa mujibu wa mikakati ya wandani hao wa Rais, wanalenga kupunguza umaarufu wa Bw Odinga katika ukanda wa Pwani na eneo la Kisii, ili kumsawiri kama kiongozi wa eneo la Luo Nyanza pekee.

Inaelezwa kuwa katika ukanda wa Pwani, maafisa hao ndio wanaopanga mikakati ya kubuniwa kwa chama huru cha kisiasa, kwa kuwafadhili magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kilifi) na Amason Kingi (Kwale).

Duru zinaeleza kwamba ni kutokana na msukumo huo ambapo Gavana Kingi alisisitiza majuzi kuhusu haja ya eneo hilo kuwa na chama chake cha kisiasa mbele ya Bw Odinga.

Baadhi ya vyama vinavyopendekezwa kufufuliwa upya ni Shirikisho na Kaddu Asili.Kwenye msururu wa mikutano aliyofanya eneo la Pwani kabla ya kutangazwa kuambukizwa virusi vya corona majuma mawili yaliyopita, Bw Odinga alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Bw Kingi, aliyesisitiza kuwa wakati umefika kwa Wapwani kuwa na chama chao ambacho kitakuwa sauti yao katika ulingo wa kitaifa.

“Maeneo mengine nchini yana vyama vyao ambavyo huwasilisha maslahi yao katika meza ya kitaifa. Wakati umefika kwa Mpwani kuwa na jukwaa litakalokuwa kama sauti yake,” akasema Bw Kingi, huku akishangiliwa na wenyeji.

Kulingana na wadadisi, kibarua kingine kinachowakabili maafisa hao wenye ushawishi serikalini ni kupunguza umaarufu wa Dkt Ruto katika ukanda wa Bonde la Ufa.

Kufikia sasa, ukanda huo umegawanyika kati ya Dkt Ruto na Gideon ambapo wote wametangaza nia ya kuwania urais 2022.Hata hivyo, wadadisi wanasema licha ya kujitokeza kuanza kuvumisha azma yake, Gideon bado hajaonyesha makali ya kisiasa, ikilinganishwa na Dkt Ruto.

“Ilivyo sasa, Dkt Ruto bado anaonekana kuwa na udhibiti na usemi mkubwa wa kisiasa Bondeni ikilinganishwa na Gideon. Itawalazimu wandani hao wabuni mikakati mipya ya kumuuza Gideon kwa wananchi,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kando na hayo, kibarua kingine ni kupenya ukanda wa Mlima Kenya, ambako ni ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta.Wadadisi wanasema kwamba ilivyo sasa, eneo hilo limegawanyika mara mbili —kati ya wale wanaomuunga mkono Rais na wale wanaohisi amewasaliti, hasa kuhusu masuala ya kilimo.

Katika mazingira hayo, wanaeleza kwamba ni vigumu kwa muungano huo kupenya bila mwonekano wa Rais Kenyatta.

“Itabidi Rais Kenyatta ajitokeze mwenyewe kuunadi muungano huo kwa wananchi, ikiwa wanasiasa hao ndio anaowapendelea kuwa warithi wake. Hilo ndilo litakalouwezesha kupenya na kukubalika kisiasa katika eneo hilo. La sivyo, huenda juhudi hizo zikabaki kuwa kibarua kizito kwa wale wanaouendesha mchakato huo,” asema Bw Muga.

Habari zinazohusiana na hii