JAMVI: Hivi anavyokuja Obado, ndiye kizibo cha Raila Nyanza?

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Gavana wa Migori Okoth Obado kumshambulia kinara wa ODM Raila Odinga imezua hisia tofauti miongoni mwa wanasiasa wa Nyanza huku baadhi yao wakiamini kuwa anatumiwa na mahasimu wa kisiasa wa kiongozi wao.

Baadhi ya wanasiasa wa ODM wanasadiki kuwa Bw Obado ni miongoni mwa magavana wanaohudumu muhula wa pili wanaotumiwa na baadhi ya wakuu serikalini kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika ngome zake.

Mbunge wa Mbita Kaskazini Millie Odhiambo na mwenzake wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma, wamempuuzilia mbali Bw Obado wakimwonya dhidi ya ‘kumdharau’ Bw Odinga.

“Raila amekuwa mgonjwa kwa zaidi ya wiki tatu sasa na amepona. Hata hivyo, watu fulani wametumia fursa hiyo kumdharau. Raila ni kiongozi wa kitaifa ambaye ushawishi wake kisiasa ni wa juu,” asema Bi Odhiambo.

Naye Bw Kaluma alisema: “Hatutavumilia watu fulani kumdharau au kutumiwa kumdhalilisha Raila.” Bw Obado, Jumapili iliyopita, alidokeza kuwa atagura ODM na kuunda chama chake atakachotumia kuwania urais 2022. Kwa mujibu wa Bw Obado, chama hicho kitasaidia watu wa Nyanza kujiondoa kwenye minyororo ya kisiasa ya Bw Odinga.

Bw Obado ambaye amekuwa akihangaishwa na msururu wa kesi mahakamani pia alipuuzilia mbali Mpango wa Maridhiano (BBI) kwamba hauna manufaa kwa Wakenya.

Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakiongoza juhudi za kutaka kurekebisha Katiba kwa kupitia Mswada wa BBI. Lakini Bw Obado Jumapili iliyopita alionekana kufurahia baada ya mswada wa BBI kukwama bungeni kutokana na kugawanyika kwa wabunge kuhusu ikiwa mswada huo unafaa kufanyiwa marekebisho au la.Bw Obado alitaka fedha zilizotengwa kwa ajili ya BBI zitumiwe kupambana na makali ya virusi vya corona.

Alisema kuwa Kenya imelemewa na mzigo wa madeni hivyo haitaweza kutekeleza mapendekezo yote ya BBI.Kiongozi wa Migori ni miongoni mwa magavana ambao wamekuwa wakipigia debe BBI kabla ya kubadili msimamo wao hivi karibuni.

“Serikali haitaweza kutoa asilimia 35 ya mapato kwa serikali za kaunti kama ilivyopendekezwa na BBI. Ikiwa asilimia 15 iliyopendekezwa na Katiba ya sasa wameshindwa, watatoa wapi asilimia 35,” akauliza Bw Obado.

Gavana wa Migori alisema kuwa ataongoza juhudi za kuunda chama kipya kitakachoshindana na ODM kinachoongozwa na Bw Odinga. Alidokeza kuwa huenda akavumisha chama cha Democratic Party (PDP) alichotumia kuwania na kushinda ugavana 2013.

Bw Obado amekuwa mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto lakini wadadisi wa siasa wanaamini kwamba tayari amemhepa na sasa anatumiwa na maafisa wa ngazi ya juu serikalini.

Kwa mujibu wa ripoti, baadhi ya wakuu serikalini wameunda njama ya kuhakikisha kuwa wanamaliza Bw Odinga kisiasa katika ngome zake.

Magavana waliotwikwa jukumu hilo ni magavana wanaohudumu mihula ya pili ambao wanapigania kupata nyadhifa serikalini baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Juhudi za Taifa Jumapili kumfikia Gavana Obado kujibu madai kwamba anatumiwa kisiasa kummaliza kisiasa Bw Odinga ziliambulia patupu huku msemaji wake Nicholas Anyuor akisema kuwa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Profesa Medo Misama, hata hivyo, anasema kuwa kumaliza ushawishi wa kisiasa wa Bw Odinga si kazi rahisi.“Wanasiasa wengi wamewahi kujitokeza kujaribu kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika eneo la Nyanza wakashindwa. Sioni iwapo Obado ambaye ushawishi wake uko katika Kaunti ya Migori pekee anaweza kumaliza Bw Odinga kisiasa,” anasema Prof Misama.

Habari zinazohusiana na hii