• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
Kivumbi kikali chaja, wandani wa Gideon waonya mahasimu

Kivumbi kikali chaja, wandani wa Gideon waonya mahasimu

Na FRANCIS MUREITHI

WANDANI wa Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi sasa wanaonya wapinzani wake kujiandaa kwa ajili ya ushindani mkali katika kinyang’anyiro cha urais.

Miongoni mwa mbinu anazolenga kutumia ni kuimarisha kampeni katika maeneo ambapo baba yake Rais mstaafu Daniel Arap Moi alikuwa na ushawishi mkubwa wakati wa uongozi wake.

Seneta wa Baringo Moi ni miongoni mwa vinara wakuu wanne wa muungano wa One Kenya Alliance ambao unajumuisha kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

“Seneta Moi ameweka mikakati kabambe ya kumwezesha kushinda urais 2022,” akasema mmoja wa wawandani wake aliyeomba jina lake libanwe kwa sababu haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya chama cha Kanu au Bw Moi.

Mahojiano yaliyofanywa na Taifa Leo yamebaini kuwa kikosi cha wataalamu ambao wameajiriwa kuboresha kampeni ya Bw Moi kinafanya kazi katika sekretariati iliyoko jijini Nairobi.

“Kazi inaendelea na tumejiandaa vyema. Uchaguzi umekaribia na shughuli ya maandalizi kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais imeshika kasi,” akasema.

Wataalamu hao wanaunda mikakati kuhusu namna Bw Moi atajipatia umaarufu nyumbani katika eneo la Bonde la Ufa ambalo linadhibitiwa na Naibu wa Rais William Ruto, kabla ya kutafuta uungwaji mkono katika maeneo mengine ya nchi.

You can share this post!

Maelfu kuenda Uingereza kabla ya marufuku kuanza

Pasaka ya hasara kwa wamiliki hoteli Pwani