• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
MAKALA MAALUM: Tohara yazua utata ikiwa ifanywe kitamaduni au kushirikisha kanisa

MAKALA MAALUM: Tohara yazua utata ikiwa ifanywe kitamaduni au kushirikisha kanisa

Na MWANGI MUIRURI

MSIMU wa tohara ambao kwa kawaida huwa muhimu kwa jamii zinazotambua desturi hiyo, sasa umegeuka kuwa kiini cha mvutano mkubwa katika jamii za eneo la Kati.

Kumezuka mvutano kati ya wazee wa jamii ya Agikuyu na wazee wa kanisa kuhusu msimu unaoendelea kwa sasa wa kutahiri wavulana wa jamii hiyo.

Kwa kawaida, msimu huo huandaliwa Desemba ya kila mwaka baada ya vijana hao kumaliza mtihani wao wa mwisho wa darasa la nane ambao hufanyika Desemba lakini kwa kuwa Covid-19 ilivuruga ratiba ya masomo, mtihani huo uliahirishwa hadi Machi, tohara nayo ikasongezwa kuambatana na hali.

Wazee katika jamii wanachukulia suala la tohara kama la kitamaduni na ambalo ni njia ya kuonyesha kuwa wamekomaa kuwa wanaume katika jamii huku kanisa likiona utaratibu wa kutahiri wavulana kuwa jambo ambalo linaonyesha msimamo wa umoja na Mungu.

Mtafaruku baina ya pande hizo mbili ulizuka baada ya kanisa kusisitiza kwamba liko na jukumu la kushirikisha tohara hiyo ndio liwajibikie jukumu la kutoa mawaidha mufti kwa vijana hao kuhusu hatua ya kutahiriwa. Pia liliazimia kuonyesha uhusiano na Mungu huku nao wazee wakishikilia kuwa ni lazima watahiriwe kwa njia za kitamaduni na mawaidha yawe kuhusu itikadi na mila za jamii.

Kauli yao

Mwenyekiti wa wazee hao wa jamii, Wachira Kiago, anasema kuwa ni lazima tohara hiyo iwe ya kuwapa vijana wa jamii hiyo mawaidha yenye mwelekeo wa kitamaduni kutoka vinywa vya wazee.

Suala hili limeibua pia mgawanyiko miongoni mwa wazazi ambao walikusudia kutahiri watoto wao.

“Mimi sitaki kuhujumu tohara ya kijana wangu iwe dini. Hili ni suala la kitamaduni. Ingawa hatuna ile hafla ya kitamaduni ya kutahirisha vijana wetu wa kiume, huwa tunawapeleka hospitalini kufanyiwa upasuaji huo mdogo, si kumpeleka kijana wangu kanisani akatahirishiwe huko. Hapo ni kuhujumu mila,” asema Mugwe Njaramba kutoka Kaunti ndogo ya Kiharu.

Makanisa mengi eneo la Kati yamezindua huduma za kuwapokea vijana hao ambao hulazwa katika mabweni kwa kipindi cha wiki mbili ambapo hutahirishwa na wanapouguza majeraha, hupewa mawaidha ya Ukristo.

Kiago anateta kuwa harakati hizo zimedunisha mila kwa kiwango kikuu “kwa kuwa unapata kijana akipelekwa kutahiri katika mabweni hayo na mama yake wakiandamana pamoja na dada zao na wanawake pia wa chama hali ambayo inadhalalisha maana kamili ya utamaduni wa tohara.”

Mipango inayoendelezwa na kanisa kuhusu tohara imekuwa ikivutia idadi kubwa ya wazazi hasa kutokana na visa vya kutisha ambavyo vilianza kushuhudiwa katika miaka michache iliyopita wakati wa tohara za kitamaduni.

Kuliwahi kutokea visa ambapo wavulana walipigwa na kuteswa kinyama na makundi ya vijana waliodai kuwa wanawafunza jinsi watakavyotakikana kuishi wakiwa watu wazima baada ya tohara.

Mbunge wa Kandara, Alice Wahome anasema kuwa tohara sasa imeibuka kuwa suala tata la kiusalama.

“Kuna majambazi ambao wameteka nyara zoezi hilo ambapo huwatembelea vijana hao na kuwapa mawaidha potovu ya kukumbatia uhaini wa kijamii,” akasema Wahome.

Wanavyosema wazazi

Kulingana naye, wazazi wengi huhisi kwamba kanisa kama taasisi kuna usalama wa kuwalinda vijana wao dhidi ya kusukumiwa kasumba za ujambazi, ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya vijana ambao hutahiri kitamaduni ambao wameishia kushambuliwa na kuuawa katika zile hali za kusajiliwa kwa magenge.

Catherine Wambui ambaye analenga kumpeleka kijana wake jandoni Aprili hii, anasema kuwa hatashawishiwa na yeyote kuhusu uamuzi atakaomfanyia mtoto wake.

“Kile tu najua ni kwamba, mtoto ni wangu na maamuzi ni yangu kuhusu jinsi zoezi hilo litatekelezwa. Lengo langu kuu ni kijana wangu atimize kigezo hicho cha kijamii ambapo ni lazima atahiriwe lakini kuhusu mjadala wa dini na mila, huo ni mvutano ambao haunisaidii,” akaeleza.

Hata hivyo, alidokeza uwezekano wa kumpeleka mtoto wake hospitalini kutahiriwa.

Anasema kuwa kanisani tohara hiyo inatozwa ada zinazotoshana na karo ya shule kwa kuwa katika kipindi hicho cha wiki mbili, gharama ni kati ya Sh10,000 na Sh15,000.

“Nikiamua kusaka kijana aliye na maadili mema kutoka kwa majirani wangu ili ampeleke huyu wangu kutahiriwa hospitalini, gharama hiyo itapungua hadi Sh600 kisha nimtunze akiwa karibu nami hadi apone. Mawaidha ya dini nitampa kwa kuwa hata mimi nimeokoka na mawaidha ya kijamii atapewa na wazee wa familia yetu kwa kuwa ndio wanaelewa kuhusu yale tunaamini kama familia,” akasema.

Anasema kuwa mvutano huo wa kanisa na wazee wa kijamii haumfai yeyote.

“Uamuzi unafaa kuwa wa wazazi, mzazi au mlezi wa mwana wala sio waliokuwa nje ya malezi hayo lakini miaka 14 baadaye, wanajipenyeza kutangaza jinsi walivyo na uwajibikaji wa maisha hayo ya kijana wa jamii hiyo na kisha baada ya kuvuna umaarufu na pesa, wanajitoa na kwenda kungoja msimu mwingine wa tohara ili warejelee mavuno,” akasema.

Mwenyekiti wa Dini Asili eneo la Mlima Kenya Askofu Julius Nyutu, anasema tohara imezingatiwa katika Bibilia haswa katika kitabu cha Mwanzo 17:13-14.

“Mungu katika maandishi hayo anaelezea waziwazi kwamba tohara ya mwanamume ni ahadi ya umoja naye katika uhai wote,” asema.

Askofu Nyutu anasema kuwa tohara ya mwanamume ni kielelezo tosha kuwa umejiingiza katika mkataba na Mungu hivyo basi huhitaji umakinifu mkuu wa kuwahamasisha watoto hao kuhusu njia za kupalilia uhusiano huo mpya na Maulana.

“Ni wakati tu vijana hao wameletwa kanisani kumsaka Mungu ambapo wanaweza wakapewa mawaidha muafaka. Ndio tunasisitiza kwamba tuchangie kuwahami vijana hao na Injili kuhusu umuhimu wa tohara na Mungu,” anaeleza.

Hata hivyo, Mshirikishi wa Muungano wa Agikuyu katika Aberdare ya Kati, James Mahinda anasema kuwa Injili hiyo ni sawa, lakini haina mashiko.

“Hatubishani kwamba Bibilia haijasema hayo yote. Tuna uwiano mmoja kwamba tohara kwa vijana wetu wa kiume ni lazima. Pale tunapohitilafiana ni kuhusu kutekwa nyara kwa mpangilio huu wa tohara ndio tupate nafasi ya kila safu, dini na mila,” anasema.

Mahinda anasema kuwa Bibilia huzingatia hali ya kiroho, mila ikizingatia kujitambua katika uhalisia wa kitamaduni.

“Tohara kwanza ni mila iliyo na desturi na hilo linafaa kushirikishwa katika jamii na wazee. Dini nayo inafaa kuandaa hafla zake zikilenga kutoa mawaidha kwa vijana hao baada ya kutahirishwa kitamaduni,” anaeleza.

Mahinda alisema kuwa wazee wa kijamii wamekuwa wakidunishwa kwa msingi kwamba wanashikilia tamaduni zilizopitwa na wakati.

Makanisa yote makuu katika eneo hilo kuanzia la Presbyterian, Katoliki na Kianglikana yako na ratiba na gharama ya kushughulikia suala la tohara.

Upande wa Serikali

Gavana Mwangi wa Iria ambaye Serikali yake hupanga hafla hizo za tohara hujumuisha wazee na pia wachungaji.

“Huwa tunapanga hafla hiyo kuwa ya pamoja ikileta mila na dini pamoja. Wazee wa kijamii hualikwa kuwapa mawaidha na wachungaji pia hualikwa. Kile cha maana ni kulinda kusiwe na ukora wa kimawaidha ambapo wengine watatoa ushauri usioambatana na dunia ya sasa. Kwa mfano, huwezi kuja hapo kama Mzee na utoe ushauri wa kuoa wake wengi, kuzaa bila mpango na kuzindua vita vya ubabe wa kiukoo na pia jinsi ukoo huu huwezi ukashirikiana na ule kwa msingi wa uhasama wa jadi,” akasema.

Aliongeza kuwa nao wachungaji hawawezi wakakubaliwa kudunisha dini zingine huku wakipigia debe wanazozipendelea.

Naibu Waziri wa Spoti, Utamaduni na Turathi za Kitaifa, Zack Kinuthia anasema kuwa “msimamo wa serikali ni kuwa tohara ni suala la kimila.”

Anasema kuwa vigezo katika Jamii za Gikuyu, Embu na Ameru kwa wanaume ni kuwa utazaliwa, utatahirishwa, utaoa na utaaga dunia. Anaongeza kuwa katika dini, matukio ni kuzaliwa, kutakaswa, kubatizwa, kuokoka na kurithi ufalme wa mbinguni.

“Lakini demokrasia ya maamuzi imewapa wazazi mwanya wa kujiamulia. Kile ningeomba mirengo hii miwili ni kwanza iwaachie wazazi nafasi ya kufanya maamuzi yao kuhusu tohara ya vijana hawa wa kiume. Mzazi akiamua anataka wake afuate mkondo wa tohara ya kanisa, ni haki yake sawa na atakayeamua wake afuate mila. Bora tu katika hali hizo zote masilahi faafu zaidi kwa maisha ya kijana huyo yatatiliwa maanani,” akasema.

You can share this post!

Watalii wafurika kupokea chanjo wenyeji wakisusia

Wachuuzi wa vyakula Ruiru walalamika