• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Serikali ijali maisha kuliko urafiki

TAHARIRI: Serikali ijali maisha kuliko urafiki

KITENGO CHA UHARIRI

MVUTANO ulioibuka kati ya Kenya na Uingereza kuhusu kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, umetoa ishara mbaya kuhusu mikakati inayoendelezwa.

Tangu mwanzoni, serikali ya Kenya ilishawishi wananchi kwamba mikakati inayoekwa inazingatia ushauri wa wataalamu lengo kuu likiwa ni kulinda maisha ya umma.

Lakini ni baada ya Uingereza kuweka masharti makali dhidi ya wasafiri wanaotoka Kenya ambapo tumeona serikali ya Kenya ikichukua hatua kali ya kuzuia uwezekano wa aina mpya ya virusi vilivyopatikana Uingereza kuingia humu nchini.

Wiki chache zilizopita, ilithibitishwa kwamba baadhi ya wanajeshi wa Uingereza ambao hufanya mazoezi yao Laikipia walipatikana wakiwa wameambukizwa aina hiyo mpaya ya virusi iliyo hatari zaidi.

Ingetarajiwa kuwa, wakati huo ndipo serikali ya Kenya ingechukua hatua kali kulinda raia wake.

Hatua ambayo imechukuliwa sasa ya kuzuia wasafiri wanaotoka Uingereza kuingia Kenya kaunzia baadaye wiki hii, imeashiria tu kwamba serikali yetu inataka kulipiza kisasi.

Kwa mtazamo wa wengi, Uingereza haikujali kama kutakuwa na mgongano wa kidiplomasia wakati ilipotangaza hatua kali ya kuzuia wasafiri wa Kenya wasiingie huko kuanzia Aprili 9.

Hii inaashiria uwezekano kuwa hilo ni taifa linalojali zaidi kulinda maisha ya wananchi wake, ijapokuwa huenda kukawa na sababu nyingine fiche zilizosababisha uamuzi huo.

Hayo ni kinyume na humu nchini kwani dhana iliyojitokeza sasa ni kuwa serikali itachukua hatua tu ikiwa imeudhika na hatua zinazochukuliwa dhidi yake, wala si kwa kuzingatia kama kuna hatari kwa umma.

Hii si tofauti na mambo tuliyoshuhudia wakati virusi vya corona vilipoanza kutambuliwa humu nchini mwaka wa 2020.

Ilichukua muda mrefu kabla serikali ianze kuweka masharti makali kwa watu waliokuwa wakiingia nchini kutoka mataifa ya kigeni ambayo wakati huo yalikuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid-19.

Tunatambua kwamba serikali ina jukumu la kufanya maamuzi kwa kuzingatia mambo mengi ikiwemo athari za kiuchumi, lakini ni muhimu maisha ya binadamu kupewa kipaumbele.

Kila mara Rais Uhuru Kenyatta anapohutubia umma kuhusu janga hili, huwa kuna sisitizo kwamba hatua zilizochukuliwa ni kwa minajili ya kulinda maisha. Hilo linafaa kuonekana kwa vitendo.

You can share this post!

Askofu Muheria awataka machifu na maafisa wa polisi...

WARUI: Ni sharti KNEC iwajibike kuondoa shaka kuhusu...