• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
WARUI: Ni sharti KNEC iwajibike kuondoa shaka kuhusu mitihani

WARUI: Ni sharti KNEC iwajibike kuondoa shaka kuhusu mitihani

Na WANTO WARUI

BARAZA la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC) limejipata katika hali tata kutokana na tetesi kuwa mtihani wa Kiingereza wa Darasa la Nane (KCPE) uliomalizika hivi maajuzi ulikuwa na sehemu ambazo zilikuwa zimenakiliwa moja kwa moja kutoka katika kitabu ambacho hakijaidhinishwa kutumiwa katika shule nchini.

Aidha, kuna sehemu ambayo inasemekana kuwa ilikuwa sawa kabisa na mtihani mmojawapo wa ile iliyofanywa nchini.

Ikiwa tetesi hizi ni za kweli, basi wananchi wanaweza kupoteza imani kwa baraza hili ambalo linatunga na kusimamia mitihani kote nchini. Mtu anaweza kujiuliza, ni kwa nini kosa kama hilo, ikiwa halikuwa kusudi, likafanywa ilhali mtihani wa kitaifa unafaa kukaguliwa vizuri na kuhaririwa ipasavyo na wasomi wenye maadili?

Mojawapo ya kanuni muhimu zaidi za utunzi wa mitihani hasa ile ya kitaifa ni kuhakikisha kuwa mtihani wowote ule hauwapi wanafunzi fulani nafasi bora ya kupita kuliko wengine. Hii ndiyo sababu kuna vitabu vya kiada vilivyopendekezwa na serikali na silabasi ambayo inafuatiliwa katika shule zote nchini.

Wizara ya Elimu huipa KNEC kazi ya kutunga mitihani kutoka katika silabasi ili iweze kubaini iwapo walimu wanafundisha wakizingatia vigezo vilivyotolewa.

Ikiwa KNEC inakiuka kaida hii, basi haina budi kulaumiwa na kukemewa kwa utendakazi duni. Itakumbukwa kuwa katika miaka ya awali pia kumekuwa na dosari nyingi katika karatasi za mitihani; ama maswali kutungwa vibaya au yale yaliyoonekana kama makosa ya uchapishaji. Mtihani wa kitaifa hautarajiwi kuwa na dosari kama hizi kamwe!

Je, kuna uwezekano kuwa baadhi ya majopo yanayotekeleza wajibu wa kutunga au kuhariri mitihani yamenaswa na mtego wa ufisadi? Kuna uadilifu wakati wa kutunga mitihani ya kitaifa? Na je, kanuni zote za utunzi wa mitihani zinazingatiwa kikamilifu?

Kutokana na tetesi hizi, wanafunzi wengi, walimu na wazazi wana wasiwasi kuhusu matokeo ya Somo la Kiingereza. Huenda shaka ikaibuka katika matokeo hayo huku wengine wakidai kuwa kuna wale wanafunzi waliokuwa wameona na hata kufanya baadhi ya sehemu za mtihani huo.

Ni jukumu la KNEC na Wizara ya Elimu kuhakikishia taifa kuwa mtihani ulikuwa sawa na ulizingatia vigezo vyote vilivyohitajika. Hakikisho kama hilo linafaa liandamane na maelezo kamili kuhusu tetesi zinazotolewa na wananchi.

Ikiwa kuna mtu au watu waliozembea katika utendakazi wao, basi hakuna shaka hatua za kisheria zinafaa kuchukuliwa dhidi ya mtu au watu hao ili kuzuia wananchi wasipoteze imani kwa KNEC.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ijali maisha kuliko urafiki

ONYANGO: Serikali ilikosea kwa kuharamisha chanjo