• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
ONYANGO: Serikali ilikosea kwa kuharamisha chanjo

ONYANGO: Serikali ilikosea kwa kuharamisha chanjo

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Wizara ya Afya kupiga marufuku kampuni za kibinafsi kuagiza chanjo ya corona kutoka ughaibuni haifai na inarejesha nyuma juhudi za kukabiliana na maradhi hayo hatari.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, Ijumaa iliyopita, alipiga marufuku kampuni au hospitali za kibinafsi kuagiza chanjo ya corona na kuitoa kwa Wakenya.

Bw Kagwe pia alifutilia mbali leseni iliyoruhusu chanjo ya Sputnik V – iliyotengenezwa nchini Urusi – ambayo ilikuwa ikitolewa humu nchini kwa Wakenya walio na uwezo wa kulipia ada ya zaidi ya Sh10,000.

Chanjo hiyo ya Urusi imekuwa ikitolewa katika Hospitali ya Bliss Westlands, Nairobi, kabla ya kuharamishwa na serikali.

Marufuku hiyo inamaanisha kuwa dozi 75,000 za chanjo ya Sputnik V zilizokuwa zimeagizwa na kampuni ya Dinlas Pharma EPZ Ltd zitauzwa katika nchi nyingine ili kuepuka hasara.

Kwa mujibu wa Bw Mutahi, chanjo ambazo hazijaidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kama vile Sputnik V, hazifai kutolewa humu nchini.

Japo haijaidhinishwa na WHO, chanjo ya Sputnik V ilithibitishwa kuwa na uwezo wa kuzuia virusi vya corona kwa asilimia 91.6. Sputnik V ni miongoni mwa chanjo chache duniani zilizo na uwezo wa kuzuia virusi vya corona kwa zaidi ya asilimia 90.

Hatua ya Kenya kungojea chanjo kuidhinishwa na WHO kabla ya kuruhusu kutumiwa humu nchini ni ithibati tosha kwamba taasisi zetu za kufanya utafiti wa chanjo na dawa zingali dhaifu.

Karibu chanjo zote zinazotumiwa kukabiliana na virusi vya corona zilianza kutumiwa katika mataifa mbalimbali kabla ya kuidhinishwa na WHO.

Kwa mfano, Uingereza iliidhinisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca Desemba mwaka jana, lakini shirika la WHO liliidhinisha chanjo hiyo Februari, mwaka huu.

Kufikia sasa Amerika haijaidhinisha chanjo ya AstraZeneca kutumiwa nchini humo licha ya kuidhinishwa na WHO.

Mkuu wa Idara ya Maradhi ya Kuambukizwa nchini Amerika Anthony Fauci majuzi alisema kuwa taifa hilo huenda lisitumie AstraZeneca.

Taasisi zetu zinahitaji kuwa na uwezo wa kuchunguza kisha kuidhinisha au kukataa chanjo bila kusubiri WHO. Chanjo zinazotumiwa katika mataifa ya Asia kama vile China, hazijaidhinishwa na WHO.

Chanjo ya AstraZeneca ambayo inaendelea kutolewa humu nchini, imekuwa ikihusishwa na visa vya kuganda kwa damu miongoni mwa baadhi ya watu wanaopewa katika mataifa kadhaa duniani.

Hivyo basi, Wakenya wanafaa kupewa fursa ya kuchagua chanjo wanayotaka.

Vile vile, serikali ya Kenya inalenga kutoa chanjo kwa Wakenya milioni 13 kufikia Juni 2023. Wengi wanaolengwa ni wahudumu wa afya, wazee wa kuanzia umri wa miaka 58 na zaidi, wagonjwa wa maradhi kama vile kisukari, maafisa wa usalama, na kadhalika.

Wakenya ambao hawako kwenye makundi hayo yanayolengwa kupewa chanjo bila malipo kufikia Juni 2023, wanafaa kuruhusiwa kujinunulia chanjo katika hospitali za kibinafsi badala ya kusubiri hadi 2024.

Lengo kuu ni kumaliza ugonjwa wa corona humu nchini na wala si kuonyeshana ubabe. Kama alivyopenda kusema mwandishi mahiri Prof Ken Walibora; ‘Tunajenga nyumba moja, hatufai kupigania fito”.

You can share this post!

WARUI: Ni sharti KNEC iwajibike kuondoa shaka kuhusu...

Mke azima polo kuoa wa pembeni